News-Details

News >Details

MZUMBE KUSHIRIKIANA NA BENKI YA DUNIA KUIMARISHA UNUNUZI ENDELEVU KATIKA MIRADI YA MAENDELEO

MZUMBE KUSHIRIKIANA NA BENKI YA DUNIA KUIMARISHA UNUNUZI ENDELEVU KATIKA MIRADI YA MAENDELEO

Chuo Kikuu Mzumbe leo, tarehe 2 Februari 2026, jijini Dar es Salaam kimezindua rasmi Mafunzo ya Kujenga Uwezo wa Ununuzi Endelevu kwa Vitengo vya Utekelezaji wa Miradi (PIUs) inayofadhiliwa na Benki ya Dunia. Mafunzo hayo yamelenga kuimarisha ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa ununuzi wa umma, ikiwa ni eneo nyeti katika mafanikio ya miradi ya maendeleo nchini. Akifungua rasmi mafunzo hayo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amesema kuwa ununuzi endelevu ni mhimili muhimu wa utawala bora na utekelezaji wenye matokeo chanya ya miradi ya maendeleo. “Ununuzi si taratibu pekee, bali ni chombo cha kimkakati cha kufanikisha matokeo ya miradi. Ununuzi unaofanyika kwa ufanisi huongeza uaminifu wa umma na kuhakikisha thamani halisi ya fedha,” alisema Prof. Mwegoha. Aliongeza kuwa uteuzi wa Chuo Kikuu Mzumbe kuwa mwezeshaji wa mafunzo hayo unaonesha imani ya Serikali na Benki ya Dunia katika uwezo wa chuo kujenga mifumo na rasilimali watu wenye weledi katika usimamizi wa miradi ya umma. Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Kamishna Msaidizi Maendeleo ya Sera Wizara ya Fedha, Bi. Emma Komba, amesema kuwa Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuboresha mifumo ya ununuzi ili kuhakikisha fedha za umma na wahisani zinasimamiwa kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia thamani ya fedha. “Mafunzo haya yanaendana na malengo ya Serikali ya kuimarisha uwajibikaji katika utekelezaji na usimamizi wa miradi ya umma. Tuna imani kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kina uwezo na utaalamu wa kusaidia kufanikisha lengo hili,” alisema Bi. Komba. Kwa upande wa Benki ya Dunia, Mwakilishi wake, Bi. Milena Stefanova, alieleza kuwa Tanzania kwa sasa inatekeleza miradi 33 inayofadhiliwa na Benki ya Dunia yenye thamani ya takribani dola za Kimarekani bilioni 8.4, hivyo ufanisi wa ununuzi una mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya maendeleo. “Pale mifumo ya ununuzi inapofanya kazi vizuri, huduma hufikishwa kwa wananchi kwa wakati barabara hujengwa mapema, shule na vituo vya afya hupata vifaa kwa wakati,” alisema Bi. Milena. Pia, Alifafanua kuwa Benki ya Dunia na Chuo Kikuu Mzumbe zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) ya kuendesha mfululizo wa mafunzo ya vitendo katika ununuzi na usimamizi wa mikataba, akisisitiza kuwa programu hiyo ni endelevu. Kwa pamoja, Serikali, Benki ya Dunia na Chuo Kikuu Mzumbe walisisitiza kuwa ushirikiano huo ni mfano bora wa jinsi taasisi zinavyoweza kushirikiana ili kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha manufaa yanawafikia wananchi kwa wakati.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None