Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu nchini, baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kampasi ya Tanga ya Chuo Kikuu Mzumbe, katika hafla iliyofanyika leo tarehe 15 Februari 2026, wilayani Mkinga, mkoani Tanga. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Serikali, uongozi wa Chuo Kikuu, wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa elimu. Akitoa ufafanuzi kuhusu mradi huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, alibainisha kuwa ujenzi wa Kampasi ya Tanga unatekelezwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia. Mradi huu ni sehemu ya jitihada za kimkakati za Serikali kuboresha ubora, upatikanaji na ulinganifu wa elimu ya juu, kwa lengo la kuchochea mageuzi ya kiuchumi na kuimarisha rasilimali watu nchini. Pia, Prof. William Mwegoha, alieleza kuwa ujenzi wa kampasi unazingatia viwango vyote vinavyotakiwa, akibainisha kuwa mradi huo una thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 12. Alifafanua kuwa kampasi hiyo itajumuisha majengo saba, yakiwemo jengo la taaluma, hosteli mbili zenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 360, bwalo la chakula lenye uwezo wa wanafunzi 450, kituo cha afya, nyumba nne za watumishi pamoja na miundombinu mingine muhimu ikiwemo tenki la maji, mfumo wa maji taka na mabwawa ya taka ngumu. Aidha, aliwasilisha mpango kabambe wa matumizi ya ardhi ya kampasi hiyo unaolenga maendeleo endelevu, kuzuia uvamizi wa ardhi na kuruhusu upanuzi wa baadaye wa miundombinu ya elimu na huduma za kijamii. Baada ya zoezi la uwekaji wa jiwe la msingi, Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba alipanda mti katika eneo la kampasi kama ishara ya ukuaji endelevu, utunzaji wa mazingira na uwekezaji wa muda mrefu katika elimu, akisisitiza kuwa maendeleo ya sekta ya elimu lazima yaende sambamba na uhifadhi wa mazingira kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo. Katika hotuba yake, Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amepongeza Uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa juhudi kubwa za kutafsiri kwa vitendo maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwekeza katika elimu ya juu kama nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa. Alisema ujenzi wa kampasi hiyo ni ushahidi wa wazi wa utekelezaji wa ahadi za Serikali kwa vitendo. “Hii siyo kampasi ya kawaida. Ni alama ya matumaini mapya kwa vijana wa Mkinga, Tanga na Tanzania kwa ujumla. Ni uwekezaji katika maarifa, ajira na uchumi wa baadaye wa Taifa letu,” amesema Waziri Mkuu, huku akitoa wito kwa wadau wote kushirikiana ili kuhakikisha kampasi hiyo inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma za elimu kwa ufanisi na ubora unaokusudiwa. Kwa upande wao, wananchi wa wilaya ya Mkinga waliishukuru Serikali kwa kuwaletea mradi huo mkubwa wa kimkakati, wakieleza kuwa uwepo wa chuo kikuu katika eneo hilo utafungua fursa mpya za maendeleo ya kijamii, kielimu na kiuchumi kwa jamii inayozunguka kampasi hiyo. Kwa kuwekwa kwa jiwe hili la msingi, Serikali imetuma ujumbe usio na shaka kwamba mustakabali wa Tanzania unajengwa kupitia elimu, maarifa na uwekezaji wa kimkakati. Kampasi ya Chuo Kikuu Mzumbe – Tanga sasa inasimama kama alama mpya ya maendeleo ya elimu ya juu, ujenzi wa uchumi imara na malezi ya kizazi chenye ushindani na mchango chanya kwa Taifa.