Kamati Tendaji ya Mradi wa kuwajengea uwezo vijana kujiajiri na kuajirika kupitia fursa za Uchumi wa Buluu ( Skills Development and Youth Employability in Blue Economy - SEBEP) unaotekelezwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imefanya ziara ya mafunzo leo tarehe 16 Februari 2026, Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu Morogoro, kwa lengo la kujifunza kwa vitendo namna taasisi ya elimu ya juu inavyopanga, kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa inayolenga kuboresha miundombinu, kuziba pengo la ujuzi na kuongeza ajira kwa vijana. Ujumbe huo ulijumuisha viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwemo Naibu Katibu Mkuu Utawala wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ndg. Amos John Henock; Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Ndg. Abeida Rashid Abdallah; Meneja wa Mradi wa SEBEP Bw. Salum Mkubwa Abdulla pamoja na wajumbe wengine. Ziara hiyo ni sehemu ya mafunzo ya vitendo yanayosimamiwa na Global Dynamics Consulting, yakilenga kuwajengea wajumbe uwezo wa kusimamia miradi ya maendeleo kwa ufanisi na uendelevu. Akizungumza wakati wa mapokezi ya ujumbe huo, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Nsubili Isaga, alifafanua kuwa Chuo kimejipanga kikamilifu kushirikisha uzoefu wake wa utekelezaji wa miradi ya elimu ya juu, akibainisha kuwa Mzumbe imekuwa ikitekeleza miradi inayolenga kuboresha miundombinu, kuongeza udahili, kuboresha mitaala na kuimarisha ajira kwa wahitimu. Akizungumza na Wajumbe wa Mradi wa SEBEP, Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Lihoya Chamwali, alieleza kuwa utekelezaji wa mradi wa HEET umetumika kama darasa la vitendo kwa wageni hao, hasa katika masuala ya ujenzi wa miundombinu, uboreshaji wa mitaala na kuandaa wahitimu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira. Kwa upande wa uhusiano na tasnia, Mratibu wa HEET katika eneo hilo Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Albogast Musabila, alieleza namna Chuo kilivyoimarisha mahusiano na taasisi za umma na binafsi ili kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi wa vitendo unaohitajika kwenye soko la ajira. Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ushughulikiaji wa Malalamiko na Uadilifu wa Mradi wa HEET, Dkt. Hanifa Massawe, alielezea mifumo inayotumika kuhakikisha malalamiko ya wadau yanashughulikiwa kwa haki, uwazi na kwa wakati, hususan katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi. Aidha, Naibu Katibu Mkuu Utawala wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ndg. Amos John Henock alitoa salamu za shukrani kwa uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe huku akieleza kuwa ziara hiyo imewawezesha wajumbe kujifunza kwa vitendo mifumo ya upangaji, usimamizi na uwajibikaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, huku akisisitiza kuwa uzoefu walioupata Mzumbe utatumika moja kwa moja kuboresha utekelezaji wa mradi wa SEBEP Zanzibar. Ziara hiyo imeonesha kwa vitendo namna Chuo Kikuu Mzumbe kinavyoishi kauli mbiu yake ya “Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu” kupitia ushirikiano na wadau wa maendeleo ya elimu.