Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, ameanza ziara rasmi ya siku tatu (3) katika Ndaki ya Mbeya kuanzia tarehe 24 hadi 27 Februari 2026 kwa lengo la kuzungumza na watumishi na wanafunzi pamoja na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika ndaki hiyo. Akiambatana na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Chuo, Prof. Mwegoha ameanza kwa kukutana na kufanya mkutano na Menejimenti ya Ndaki ya Mbeya, ambapo alipokea taarifa ya maendeleo iliyowasilishwa na Rasi wa Ndaki, Prof. Henry Mollel, pamoja na kufanya majadiliano ya kina kuhusu hali ya maendeleo ya Ndaki. Akizungumza katika mkutano na Menejimenti ya Ndaki hiyo, Prof. Mwegoha aliipongeza Menejimenti ya Ndaki ya Mbeya kwa kusimamia usalama wa Ndaki pamoja na kusimamia masuala ya taaluma. Pia alisifu juhudi zinazofanywa katika kusimamia miradi ya maendeleo na kuhimiza kuendelea kufanya kazi kwa mshikamano ili kufikia malengo ya chuo. “Naipongeza menejimenti ya Ndaki ya Mbeya ikiongozwa na Rasi wa Ndaki, Prof. Henry Mollel kwa kuhakikisha Ndaki ipo salama, ziara hii ni tamaduni bora kwa ajili ya kufahamu fursa na changamoto kwenye Ndaki za Chuo na kuja na maono yatakayochochea fursa hizo kuwa mafanikio na suluhisho za changamoto kwa ajili ya maendeleo ya taasisi yetu.” Alisema Prof. Mwegoha. Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya Ndaki ,Rasi wa Ndaki ya Mbeya Prof. Henry Mollel alieleza juu ya mafanikio ya Ndaki yaliyopatikana katika nyanja za taaluma, utafiti, ubunifu, changamoto zinazoikabili Ndaki pamoja na mikakati ya kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia na kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo. Aidha, Makamu Mkuu alipata nafasi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea katika ndaki, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya usambazaji maji safi, ujenzi wa kiwanja cha mpira pamoja na Zahanati ya Ndaki ya Mbeya. Alieleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo na kusisitiza ubora na kukamilika kwa wakati. Katika hatua nyingine ya ziara hiyo, Prof. Mwegoha amekabidhiwa jengo lililouzwa na benki ya Maendeleo kwa Ndaki ya Mbeya katika eneo jirani ikiwa ni hatua ya Ndaki hiyo ya kuboresha huduma za uendeshaji na taaluma, likitarajiwa kuongeza ofisi, vyumba vya mihadhara na huduma kwa wanafunzi. Ziara hiyo ni sehemu ya ratiba ya uongozi wa Chuo ya kutembelea vitivo na ndaki zake kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa majukumu na kuhakikisha kuwa Ndaki ni salama kwa ajili ya maendeleo ya taasisi.