Katika jitihada za kufanikisha hatua za mwisho za utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaolenga kuimarisha ubora, ufanisi na mchango wa elimu ya juu katika maendeleo ya taifa, Chuo Kikuu Mzumbe kimeratibu mafunzo kuhusu Maandalizi ya Kukabidhi na Kufunga rasmi Mradi kwa waratibu wa mradi huo, kwa lengo la kuhakikisha taratibu zote za ukamilishaji na makabidhiano yanazingatiwa kikamilifu kabla ya mradi kufungwa rasmi. Mafunzo hayo ya siku tano yanafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo Kikuu Mzumbe – Kampasi Kuu Morogoro, na yamefunguliwa rasmi leo tarehe 23 Februari 2026, yakihusisha Waratibu wa Mradi wa HEET Chuo Kikuu Mzumbe, akiwemo Naibu Mratibu wa Mradi, Dkt. Lihoya Chamwali, ambao walipata fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto mbalimbali za usimamizi wa mradi pamoja na mbinu bora za kuzitatua kwa weledi. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Gabriel Komba alieleza kuwa mafanikio ya mradi hayapimwi kwa kukamilika kwake pekee, bali pia kwa namna mradi unavyokabidhiwa na kufungwa kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa na kitaasisi. “Hatua ya ukabidhi na kufunga mradi ni muhimu katika kuhakikisha kuwa malengo ya mradi yanatimia kikamilifu na kwamba rasilimali zilizotumika zimetoa thamani halisi kwa kiwango kilichokusudiwa,” alisema Prof. Komba. Mafunzo hayo yanawezeshwa na wataalamu wa mradi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ambao walitoa mwanga kuhusu taratibu, mbinu bora na mahitaji ya kitaalamu yanayopaswa kuzingatiwa katika hatua za mwisho za utekelezaji wa Mradi wa HEET. Akiwasilisha mada kuhusu Awamu za Utekelezaji wa Miradi ya Ujenzi na Maendeleo ya Mradi, Msanifu Majengo Bw. Dickson Haule alisisitiza umuhimu wa kufuatilia kwa kina kila hatua ya mradi kuanzia mwanzo hadi mwisho, ili kuhakikisha viwango vya kitaaluma, ubora na ufanisi vinatimizwa. “Uelewa sahihi wa awamu za utekelezaji wa mradi ni nguzo muhimu katika kusimamia rasilimali kwa ufanisi na kuzuia changamoto zisizotarajiwa wakati wa utekelezaji,” alieleza Bw. Haule. Kwa upande wake, Mhandisi Hanington Kagiraki aliwasilisha mada kuhusu Maandalizi ya Kukamilisha na Kukabidhi Mradi akifafanua taratibu muhimu katika hatua ya ukamilisho, ikiwemo ukaguzi wa kazi zilizotekelezwa, maandalizi ya nyaraka za kiufundi, pamoja na taratibu za mwisho za kimkataba na usimamizi wa baada ya ukabidhi. Kwa ujumla, mafunzo hayo yameelezwa kuwa hatua muhimu katika kujenga uwezo wa waratibu wa Mradi wa HEET, kuhakikisha hatua za mwisho za utekelezaji wa mradi huu wa kitaifa zinafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia vipaumbele vyake vya msingi, na hivyo kuweka msingi imara wa kuleta athari chanya katika utoaji wa elimu ya juu, utafiti na ubunifu nchini Tanzania.