Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kujiimarisha kama kitovu cha tafiti zenye mwelekeo wa kijamii na kimazingira baada ya kuendesha kikao cha siku tano kilichowahusisha watafiti wa ndani na wa kimataifa kwa ajili ya kupanga utekelezaji wa mradi mpya wa utafiti wa mabadiliko ya tabianchi unaojulikana kama From Lab2Life and Back. Mradi huu unaolenga sayansi ya jamii katika mabadiliko ya tabianchi na maji, hususan athari za mafuriko katika jamii zinazokumbwa na changamoto hizo. Kikao hicho kilifanyika tarehe 08 hadi 12 Februari 2026 katika Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe mkoani Morogoro, na kuwakutanisha watafiti kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) pamoja na Chuo Kikuu cha Antwerp kupitia Taasisi ya Sera za Maendeleo (IOB). Ushirikiano huu wa kitaaluma unalenga kuzalisha tafiti shirikishi zitakazotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili, huku zikilenga kutoa mchango wa moja kwa moja katika uelewa wa mabadiliko ya tabianchi na usimamizi wa rasilimali za maji. Lengo kuu la kikao hicho lilikuwa ni kujadili mwelekeo wa uendeshaji wa tafiti za mradi huo mpya, ikiwemo mbinu za utafiti, maeneo ya utafiti, mgawanyo wa majukumu kwa taasisi washirika, pamoja na mifumo ya ufuatiliaji na tathmini itakayohakikisha tafiti zinazofanyika zinaakisi uhalisia wa mabadiliko ya tabianchi katika jamii zinazolengwa. Aidha, washiriki walijadiliana namna bora ya kuhakikisha tafiti hizi zinatoa matokeo yanayoweza kutumika katika kupanga mikakati jumuishi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Katika hatua ya awali ya maandalizi, timu ya watafiti ilifanya ziara ya kikazi katika ofisi za Bodi ya Bonde la Maji la Wami / Ruvu kwa lengo la kuomba ushirikiano wa kitaalamu na kupata takwimu muhimu zitakazosaidia katika ufuatiliaji wa mwenendo wa maji na tathmini ya mafuriko katika maeneo ya utafiti, hususan katika bonde la Mto Wami. Hii ilikuwa hatua muhimu ya kuhakikisha kuwa tafiti zinazofanyika zinazingatia mazingira halisi na changamoto zinazokabili jamii. Mradi wa From Lab2Life and Back unaweka mkazo katika sayansi ya jamii katika mabadiliko ya tabianchi na maji, ambapo mojawapo ya athari kuu za mabadiliko hayo ni mafuriko. Katika hatua ya awali, tafiti za mradi huo zitatekelezwa katika Wilaya ya Mvomero, zikianzia eneo la Turiani, ambalo limekuwa likikumbwa mara kwa mara na changamoto za mafuriko zinazowaathiri wananchi, uzalishaji wa kilimo, na miundombinu ya kijamii. Washirika wanakusudia kuzalisha ushahidi wa kisayansi utakaosaidia kuimarisha uelewa wa athari za mabadiliko ya tabianchi katika jamii, hususan mafuriko, na kuwezesha upangaji wa mikakati jumuishi na endelevu ya usimamizi wa rasilimali za maji kwa manufaa ya wananchi na wadau wa maendeleo.