News-Details

News >Details

MZUMBE YAFANYA MHADHARA WA UMMA KUHUSU USIMAMIZI WA RASILIMALI

MZUMBE YAFANYA MHADHARA WA UMMA KUHUSU USIMAMIZI WA RASILIMALI

Chuo Kikuu Mzumbe kimefanya Mhadhara wa umma tarehe 28 Januari, 2026 ulioandaliwa na Kitivo Cha sayansi ya jamii na kuwakutanisha wanataaluma, watafiti, pamoja na wanafunzi wa shahada mbalimbali za Umahiri na Uzamivu kutoka Kampasi Kuu ya Morogoro. Mhadhara huo ulikuwa na lengo la kujadili masuala mtambuka ya usimamizi wa rasilimali za pamoja kwa kuzingatia changamoto na fursa zilizopo katika mazingira ya sasa ya maendeleo endelevu. Akiwasilisha mada katika mhadhara huo iliyohusu “Kuziba Pengo la Utawala kupitia Muunganiko wa Sekta za Maji, Nishati na Chakula katika Usimamizi wa Rasilimali za Pamoja,” Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini, Dkt. Letaro Phali, alieleza kuwa changamoto nyingi za kiutawala katika nchi zinazoendelea zinatokana na mifumo ya kisekta inayofanya kazi kwa kutengana badala ya kushirikiana. Alisisitiza kuwa muunganiko wa sekta hizo tatu ni muhimu katika kuhakikisha matumizi bora, endelevu na yenye usawa wa rasilimali za pamoja. “Hakuna sekta inayoweza kusimamia rasilimali za pamoja kwa ufanisi bila kushirikiana na sekta nyingine. Maji, nishati na chakula ni mifumo inayotegemeana, hivyo sera na maamuzi ya kiutawala yanapaswa kuzingatia uhusiano huo ili kuleta maendeleo jumuishi,” alisema Dkt. Phali. Mhadhara huo umekuwa na mafanikio makubwa kwa washiriki, kwani uliwapa nafasi ya kujifunza kwa kina kuhusu dhana ya muunganiko wa sekta, kubadilishana uzoefu wa kitaaluma, pamoja na kujadili tafiti na mifano halisi ya usimamizi wa rasilimali kutoka ndani na nje ya Afrika. Washiriki walipata fursa ya kuuliza maswali, kutoa maoni, na kujadili changamoto za kiutawala zinazojitokeza katika sekta hizo, hali iliyochochea mjadala mpana na wenye tija. Pia, mhadhara huo umeongeza kwa kiasi kikubwa uelewa na upeo wa maarifa miongoni mwa jumuiya ya Mzumbe, hususani kwa wanafunzi, jambo lililodhihirisha nafasi yake kama kitovu muhimu cha tafakuri za kitaaluma na majadiliano ya masuala ya maendeleo endelevu. Kupitia uandaaji wa majukwaa ya kielimu yanayolenga kujadili na kutatua changamoto halisi za jamii, taasisi hiyo inaendelea kuishi na kutafsiri kwa vitendo kauli mbiu yake ya “Tujifunze kwa maendeleo ya watu.”

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None