Ushirikiano wa kitaaluma kati ya Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo Kikuu cha Ghent cha nchini Ubelgiji umeendelea kuzaa matokeo chanya kufuatia kuandaliwa kwa mafunzo maalumu ya uchambuzi wa data na teknolojia za Akili Unde kwa wataalamu kutoka Wizara, Idara na Wakala za Serikali (MDAs), mafunzo yaliyofanyika kuanzia Februari 24 hadi 27, 2026 jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kimataifa wa Data2Info unaolenga kuboresha uwezo wa taasisi za umma katika matumizi ya takwimu kwa maendeleo endelevu ya uchumi. Mafunzo hayo yamewakutanisha wataalamu kutoka wizara na taasisi mbalimbali za serikali zikiwemo Wizara ya Madini, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Afya, Wizara ya Maji pamoja na Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, sambamba na taasisi za udhibiti, utafiti na mifuko ya hifadhi ya jamii. Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, Mratibu wa Mradi wa Data2info Dkt. Almasi Maguya alieleza kuwa lengo kuu ni kuwajengea wataalamu wa serikali ujuzi wa kisasa wa uchambuzi wa data unaoweza kusaidia taasisi kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi wa takwimu. “Mafunzo haya yanajikita katika maeneo muhimu kama misingi ya kuandika programu za kompyuta kwa kutumia Python, mbinu za uchambuzi wa data, matumizi ya Machine Learning, pamoja na uelewa wa Large Language Models. Maarifa haya ni muhimu kwa taasisi zetu katika kufanya maamuzi sahihi yanayotokana na uchambuzi wa data,” alisema Dkt. Maguya. Kupitia mafunzo hayo, washiriki wamepata fursa ya kujifunza mada mbalimbali muhimu ikiwemo misingi ya takwimu (Introductory Statistics), mbinu za uchambuzi wa data, matumizi ya programu za kompyuta kwa lugha ya Python, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa kama Akili Mnemba (Artificial Intelligence) na Machine Learning katika kuchakata na kuchambua taarifa. Mbali na kujifunza mbinu za kitaalamu, washiriki pia wanapata nafasi ya kubadilishana uzoefu kuhusu changamoto zinazojitokeza katika usimamizi na uchambuzi wa data ndani ya taasisi zao, hatua ambayo inalenga kusaidia kubuni suluhisho za pamoja zitakazoboresha matumizi ya data katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo. Kwa mujibu wa waandaaji wa mafunzo hayo, ushiriki mpana wa wataalamu kutoka sekta mbalimbali za serikali unasaidia kuimarisha majadiliano na kujenga mtandao wa kitaalamu utakaowezesha ushirikiano katika matumizi ya data kwa ajili ya kufanya maamuzi yenye tija kwa maendeleo ya taifa. Washiriki wa mafunzo hayo wamehimizwa kuendelea kutumia na kusambaza maarifa waliyoyapata kwa wenzao katika taasisi zao ili kuongeza ufanisi katika uchambuzi na matumizi ya data, hatua inayotarajiwa kuimarisha utamaduni wa kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi wa takwimu katika taasisi za umma.