Katika hatua ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha sekta ya elimu, Chuo Kikuu Mzumbe kimekabidhi vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni tano kwa Shule ya Msingi Vikenge, Morogoro, leo tarehe 19 Machi 2026 kwa lengo la kusaidia ukamilishaji wa darasa jipya na kupunguza msongamano wa wanafunzi. Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Hawa Tundui, amesema msaada huo umetolewa baada ya kupokea ombi kutoka kwa uongozi wa shule hiyo uliobainisha changamoto ya uhaba wa madarasa. Amesema kupitia msaada huo, vifaa mbalimbali ikiwemo saruji, mbao na rangi vimekabidhiwa kwa lengo la kukamilisha darasa linalojengwa, huku akisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya chuo ya kurejesha kwa jamii (outreach policy). “Mbali na msaada wa vifaa, tupo tayari pia kushirikiana na jamii kwa kutoa mafunzo katika nyanja mbalimbali ikiwemo sheria, utawala na ujasiriamali, pale tutakapohitajika,” amesema Prof. Tundui. Naye Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi wa chuo hicho, Nicolaus Mtui, amesema ushirikiano kati ya taasisi za elimu na jamii ni nguzo muhimu ya maendeleo endelevu, akiahidi kuwa chuo kitaendelea kushirikiana na shule na taasisi nyingine zenye uhitaji. Awali, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Vikenge, Mwl. John Joseph, ameeleza kuwa wanafunzi wengi walikuwa wakisomea katika mazingira ya msongamano mkubwa. “Kwa msaada huu, si tu tunajenga darasa, bali tunajenga mustakabali wa watoto wetu. Tulikuwa na madawati mengi tuliyopata awali, lakini hatukuwa na vyumba vya kutosha. Sasa tunaanza ukurasa mpya,” ameeleza Mwl. John. Ameongeza kuwa kasi ya ujenzi inaendelea vizuri na matarajio ni kwamba ndani ya wiki mbili darasa hilo litakuwa tayari kutumika, hatua itakayopunguza changamoto ya uhaba wa nafasi za kujifunzia. Makabidhiano hayo yameonekana kuwa chachu ya mabadiliko kwa shule hiyo, yakitoa taswira ya namna ushirikiano kati ya taasisi za elimu na jamii unavyoweza kuleta matokeo chanya na endelevu.