News-Details

News >Details

MZUMBE YAENDESHA MAFUNZO KUHUSU ULINZI WA TAARIFA NA USIMAMIZI WA NYARAKA

MZUMBE YAENDESHA MAFUNZO KUHUSU ULINZI WA TAARIFA NA USIMAMIZI WA NYARAKA

Katika jitihada za kuimarisha uelewa wa kitaaluma kuhusu utunzaji salama wa taarifa na usimamizi bora wa kumbukumbu katika taasisi, Chuo Kikuu Mzumbe kimeandaa Mafunzo ya ya siku tatu ya Ulinzi wa Taarifa na Usimamizi wa Nyaraka Nchini Tanzania kwa kuzingatia sheria, usalama na mbinu bora . Mafunzo hayo yamefanyika leo tarehe 04 Machi 2026 katika Hoteli ya Edema, mkoani Morogoro, yakilenga kuwajengea washiriki maarifa na ujuzi unaohitajika katika kusimamia taarifa na kumbukumbu za taasisi kwa kuzingatia matakwa ya kisheria na kitaaluma. Akifungua mafunzo hayo, Mtiva wa Kitivo cha Sheria wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Seraphina Bakta, alisisitiza umuhimu wa taasisi za umma na binafsi kuzingatia mifumo madhubuti ya utunzaji wa taarifa na kumbukumbu ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji wa majukumu yao. Alieleza kuwa mabadiliko yanayoletwa na maendeleo ya teknolojia ya habari yanahitaji taasisi kuwa na maarifa ya kutosha kuhusu sheria, kanuni na mbinu zinazosaidia kulinda taarifa muhimu pamoja na kusimamia nyaraka kwa ufanisi. “Katika zama hizi za maendeleo ya teknolojia ya habari, ulinzi wa taarifa na usimamizi sahihi wa nyaraka si chaguo bali ni wajibu. Ni muhimu kwenu kutumia mafunzo haya kujenga uwezo utakaozisaidia taasisi zenu kuimarisha uwajibikaji, usalama wa taarifa na ufanisi wa utendaji kazi,” alisema Dkt. Bakta. Kwa upande wake, Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Mhadhiri na Wakili kutoka Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Lukiko Lukiko, aliwasilisha mada kuhusu “Utangulizi wa Ulinzi wa Taarifa na Usimamizi wa Nyaraka” pamoja na “Mfumo wa Kisheria na Kiudhibiti wa Ulinzi wa Taarifa na Usimamizi wa Nyaraka.” Mada hizo zililenga kuwajengea washiriki uelewa mpana kuhusu dhana ya kulinda taarifa, umuhimu wa utunzaji wa kumbukumbu katika taasisi pamoja na wajibu wa kufuata misingi ya kisheria na kanuni za udhibiti katika matumizi na uhifadhi wa taarifa. Dkt. Lukiko alieleza kuwa uwepo wa mifumo bora ya kuhifadhi na kusimamia kumbukumbu unasaidia taasisi kufanya maamuzi sahihi, kulinda taarifa nyeti na kupunguza hatari zinazoweza kusababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya taarifa. “ Ni muhimu kwa taasisi kujenga utamaduni wa kusimamia nyaraka kwa weledi na kuzingatia sheria za ulinzi wa taarifa, kwani kufanya hivyo kunasaidia kulinda maslahi ya taasisi, kuongeza uwajibikaji na kuimarisha imani ya umma kwa taasisi husika,” alieleza Dkt. Lukiko. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 06 Machi 2026 na yanawakutanisha washiriki mbalimbali wakiwemo Maafisa Rasilimali Watu, Maafisa TEHAMA, Wasimamizi wa Kumbukumbu pamoja na Waandishi Waendesha Ofisi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA). Kupitia programu hiyo ya mafunzo, washiriki wanapata fursa ya kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu za kisasa za usimamizi wa taarifa na kuimarisha uwezo wao wa kitaaluma katika kuhakikisha taasisi wanazotoka zinaendesha shughuli zake kwa kuzingatia misingi ya sheria, uwajibikaji na usalama wa taarifa.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None