News-Details

News >Details

MZUMBE YAPONGEZWA NA COSTECH KWA UFANISI WA MRADI WA STE&GRL

MZUMBE YAPONGEZWA NA COSTECH KWA UFANISI WA MRADI WA STE&GRL

Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kudhihirisha ubora wake katika tafiti na ubunifu baada ya wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), wakiongozwa na Dkt. Zebedayo Baniga, kuonesha kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa STE&GRL wakati wa ziara ya tathmini iliyofanyika Kampasi Kuu Morogoro tarehe 31 Machi 2026. Ziara hiyo ya tathmini ililenga kujionea hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo unaojikita katika kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia, mazingira na masuala ya kijinsia kwa maendeleo endelevu. Katika ukaguzi huo, timu ya wataalamu imepongeza kazi kubwa inayofanywa na watafiti pamoja na wasimamizi wa mradi, ikibainisha kuwa utekelezaji wake unaonesha mwelekeo sahihi na matokeo yenye tija yanayoonekana. Mradi wa STE&GRL unatekelezwa katika Wilaya ya Tanganyika, Mkoa wa Katavi, ukilenga kunufaisha wafugaji na wakulima wafugaji katika vijiji vya Sibwesa, Mnyagala, Lwega na Mpembe. Kupitia utekelezaji wake, mradi unalenga kuchochea maendeleo endelevu kwa kuzingatia changamoto za mazingira, mabadiliko ya tabianchi pamoja na ustawi wa jamii hizo. Lengo kuu la mradi huu ni kuelewa hali ya mazingira baada ya mabadiliko ya makazi (post-migration environment) na kuanzisha afua zitakazopunguza athari hasi kwa maisha endelevu ya jamii katika Wilaya ya Tanganyika. Ili kufanikisha hilo, mradi unatekeleza malengo mahsusi yanayojumuisha tathmini ya athari za mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa jamii za wafugaji na wakulima wafugaji, kuchambua athari za muda mfupi na mrefu za uhamaji kwa mifumo ya ikolojia na hali za kiuchumi, pamoja na kupima ufanisi wa afua zilizopo katika kukuza maisha endelevu na usimamizi bora wa mifugo. Akizungumza wakati wa tathmini hiyo, kiongozi wa ujumbe huo, Dkt. Zebedayo Baniga, alisema kuwa ameridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa mradi huo, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi hizo ili kufikia malengo yaliyowekwa kwa ufanisi zaidi. Kwa upande wa mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa, mradi umefanikiwa kuandaa na kuwasilisha taarifa ya awali (Inception Report), kushiriki katika uzinduzi wa kitaalamu wa miradi ya COSTECH, pamoja na kufanya uzinduzi rasmi wa mradi (kick-off). Vilevile, utafiti wa msingi (baseline survey) umefanyika katika maeneo ya utekelezaji, huku juhudi za kujenga uwezo wa rasilimali watu zikiendelea kupitia udhamini na ushirikishwaji wa wanafunzi wa Shahada za Umahiri (MSc) na Uzamivu (PhD). Katika hatua nyingine, ujumbe huo ulizungumza na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, ambapo uliwasilisha mrejesho chanya kuhusu maendeleo ya mradi huo. Wataalamu hao walieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana yanaakisi mwenendo wa chuo katika kukuza tafiti na ubunifu unaochangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. Mradi wa STE&GRL unatarajiwa kuendelea kutoa mchango mkubwa katika kukuza matumizi ya sayansi na teknolojia pamoja na kuimarisha maendeleo jumuishi, hususan katika kukabiliana na changamoto za mazingira, mabadiliko ya tabianchi na ustawi wa jamii. Matokeo ya ziara hiyo yanaashiria hatua madhubuti kuelekea mafanikio makubwa ya mradi, huku yakitoa msukumo kwa timu ya utekelezaji kuendelea kubuni na kutekeleza mikakati yenye tija zaidi kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

None
None
None
None