Katika kuendeleza mapinduzi ya elimu kwa kutumia Teknolojia ya Akili Mnemba, Chuo Kikuu Mzumbe kimewakutanisha wadau wake leo, Aprili 14, 2026, katika Kampasi Kuu Morogoro, kwa lengo la kujadili tathmini ya utekelezaji, mafanikio na mwelekeo wa miradi ya AI4STEM, Data2Info na Global Citizenship. Akiwasilisha mwelekeo wa Mradi wa Data2Info, Mratibu wake, Dkt. Almasi Maguya, alieleza kuwa mradi huo unalenga kuboresha ukusanyaji, uchakataji na matumizi ya takwimu sahihi ili kusaidia maamuzi yenye ushahidi. Alifafanua kuwa kupitia mradi huo, taasisi zimeanza kunufaika na mifumo bora ya usimamizi wa taarifa, hali inayochangia kuongeza ufanisi katika upangaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo. Kwa upande wa Mradi wa AI4STEM, Dkt. Tupokigwe Isagah alibainisha kuwa mradi huo unalenga kuleta mageuzi katika elimu ya sayansi na teknolojia kupitia kuanzishwa kwa Kituo cha Utafiti na Ubunifu wa Akili Mnemba (CAIRI), kukuza uwezo wa utafiti na ubunifu, pamoja na kujenga jamii inayotumia na kunufaika na teknolojia ya AI. Alitaja mafanikio yaliyofikiwa kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa watafiti wa ngazi ya juu, ushiriki katika maboresho ya mwongozo wa matumizi ya Akili Mnemba katika elimu chuoni, pamoja na kuanzishwa kwa CAIRI. Naye Bw. Edger Rutatola, akiwasilisha kuhusu mradi wa Global Citizenship, alieleza kuwa unalenga kuwaandaa wanafunzi kuwa raia wa kimataifa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya akili mnemba, hususan katika kuboresha umahiri wa lugha ya Kiingereza kwa wanafunzi wa shule za msingi nchini Tanzania. Aidha Bw. Rutatola aliongeza kuwa mradi huo unatarajia kuboresha zana za kufundishia zinazotumia Akili Mnemba, kuboresha ufaulu wa somo la Kiingereza, kuchochea maboresho ya mitaala yanayotokana na tafiti, pamoja na kuimarisha uwezo wa wataalamu wa Chuo Kikuu Mzumbe katika kubuni suluhisho bunifu zenye tija kwa jamii. Katika mjadala, wadau walisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya chuo, serikali na sekta binafsi, pamoja na kuweka mifumo imara ya kifedha na kiutendaji ili kuhakikisha uendelevu wa miradi hiyo na matokeo yake kwa muda mrefu. Mwelekeo huo unaashiria mustakabali mpya wa elimu unaotegemea teknolojia bunifu katika kutatua changamoto za kijamii na kielimu.