News-Details

News >Details

KONGAMANO LA AFYA MZUMBE LACHOCHEA UWAJIBIKAJI WA KIAFYA KWA VIJANA

KONGAMANO LA AFYA MZUMBE LACHOCHEA UWAJIBIKAJI WA KIAFYA KWA VIJANA

Katika kuendeleza jitihada za kukuza ustawi wa wanafunzi na jamii, Chuo Kikuu Mzumbe kimefanya Kongamano la Afya lililowakutanisha wanafunzi na wadau mbalimbali wa sekta ya afya, likiwa jukwaa la utoaji elimu, huduma na uhamasishaji kuhusu masuala tofauti ya kiafya, leo Aprili 18, 2026, katika Kampasi Kuu ya Chuo hicho mkoani Morogoro. Akifungua rasmi kongamano hilo, Mwakilishi wa Amidi wa Skuli ya Utawala wa Umma na Menejimenti Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Godfrey Kacholi, aliwahimiza vijana kutambua thamani ya afya zao na kuchukua hatua madhubuti za kujikinga na magonjwa. Aidha, Dkt. Kacholi alieleza kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa, hivyo afya yao ni msingi wa maendeleo endelevu, akisisitiza kuwa elimu ya afya ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto za kiafya zinazoongezeka. Naye Mkurugenzi wa Huduma za Afya wa Chuo, Dkt. Nyangara Rajabu, alieleza kuwa kongamano hilo limeandaliwa mahsusi kuwafikia wanafunzi na jamii kwa kutoa huduma mbalimbali zikiwemo uchangiaji wa damu, upimaji wa afya na elimu kuhusu magonjwa tofauti ikiwemo VVU. Pia, alisisitiza kuwa uchangiaji damu ni tendo la uokoaji maisha na kuhimiza ushiriki mpana wa wanafunzi katika zoezi hilo. Kwa upande wake, Mtoa mada mkuu ambaye pia ni Mtaalamu wa Afya ya Akili, Dkt. Pascal Kang’iria, alieleza kwa kina dhana ya afya ya akili na nafasi yake katika maisha ya kila siku. Alifafanua kuwa afya ya akili si tu kutokuwepo kwa ugonjwa, bali ni uwezo wa mtu kujitambua, kudhibiti hisia na kukabiliana na changamoto za maisha kwa ufanisi, huku akisisitiza umuhimu wa uelewa wa hisia katika kuboresha mahusiano na utendaji wa kila siku. Aidha, wataalamu wengine waliwasilisha mada mbalimbali zilizoangazia nyanja tofauti za afya. Dkt. Mohamed Ayub alizungumzia masuala ya utoaji mimba na magonjwa ya zinaa, akibainisha umuhimu wa uelewa wa kisheria na kiafya, naye Dkt. Stephen Mwaikambo alieleza umuhimu wa uzazi wa mpango kwa vijana katika kupanga maisha yao, huku Dkt. Athuman Mlendemla akitoa elimu kuhusu VVU, namna vinavyoambukizwa na njia za kujikinga. Vilevile, Bi. Tunukiwa Kasambala kutoka MyService kwa kushirikiana na TACAIDS alieleza kuhusu uwepo wa mashine ya kiotomatiki ya utoaji kondomu na vifaa vya kujipima VVU chuoni hapo, akibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za kinga kwa njia salama ya siri na ya haraka. Kwa ujumla, kongamano hilo limeweka msisitizo mkubwa katika uwajibikaji binafsi wa afya, likiwa sehemu ya juhudi za Chuo Kikuu Mzumbe katika kuandaa wanafunzi wenye uelewa mpana na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi yanayolinda na kuimarisha ustawi wa afya zao.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None