Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kuonyesha kwa vitendo uwezo wake katika kuzalisha tafiti zenye tija na mchango chanya katika maendeleo ya taifa, kufuatia mafanikio ya Bw. Lubango Mayenga, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka Skuli ya Biashara, ambaye ametetea tasnifu yake kwa mafanikio tarehe 27 Aprili 2026 katika Kampasi Kuu ya Morogoro. Utetezi huo ulifanyika mbele ya jopo la watahini lililoongozwa na Profesa Ernest Kihanga, ambapo Bw. Mayenga aliwasilisha utafiti wake wenye mada “Vichocheo vya Wateja Kukubali Huduma za Benki za Kiislamu Nchini Tanzania.” Katika utafiti huo, Bw. Mayenga alichambua kwa kina mambo mbalimbali yanayoathiri maamuzi ya wateja kukubali na kutumia huduma za benki za Kiislamu, yakiwemo kiwango cha uelewa wa huduma hizo, nafasi ya imani za kidini, uaminifu kwa taasisi za kifedha, pamoja na ubora wa huduma zinazotolewa. Akiwasilisha matokeo ya utafiti wake, Bw. Mayenga alieleza kuwa kiwango cha uelewa miongoni mwa jamii bado ni changamoto inayoathiri upokeaji wa huduma hizo. Aidha, alisisitiza kuwa elimu ya kifedha kwa umma ni muhimu katika kuongeza ushiriki wa wateja, sambamba na kuboresha mifumo ya utoaji huduma ndani ya taasisi za kifedha ili kuongeza uaminifu na imani kwa huduma hizi. Tasnifu hiyo ilisimamiwa na Dkt. Moshi James (Msimamizi Mkuu) pamoja na Dkt. Matha Maziku (Msimamizi Msaidizi), ambao walitoa mwongozo wa karibu na ushauri wa kitaaluma uliomwezesha mtafiti kukamilisha utafiti wake kwa mafanikio makubwa na viwango vya juu vya kitaaluma. Baada ya majadiliano ya kina, Profesa Ernest Kihanga, Mwenyekiti wa jopo la watahini, alimpongeza Bw. Mayenga kwa kuonesha umahiri mkubwa katika uchambuzi wa kitaaluma, uwezo wa kujenga hoja, na kujibu maswali kwa ufanisi, akibainisha kuwa utafiti huo una mchango muhimu katika kuimarisha sekta ya fedha na kuongeza uelewa wa huduma za benki za Kiislamu nchini. Mafanikio haya yanaakisi mchango endelevu wa Chuo Kikuu Mzumbe katika kukuza tafiti zenye ubora na manufaa kwa jamii, na kuendelea kuwa chachu ya maendeleo endelevu nchini Tanzania. https://www.instagram.com/p/DXpOBrDguA7/?igsh=MWc0ZWs5cHpqaDY3ZA==