Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Taasisi ya Taaluma za Maendeleo (IDS) chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), kimeandaa warsha kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Warsha hii imefanyika Kampasi Kuu, Morogoro, tarehe 12 Februari 2025, kwa ajili ya kuongeza uelewa wa jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi, vyanzo vyake, na suluhisho endelevu. Washiriki wa warsha hii walikuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Kwanza ya Menejimenti ya Mazingira, ambao walipata fursa ya kujadili mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto za kimazingira kwa maendeleo ya sasa na ya baadaye. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Dkt. Editha Ndunguru, Mratibu wa Mradi wa HEET upande wa mazingira, alisisitiza umuhimu wa elimu ya tabianchi katika kuhimili athari zake na kuchukua hatua muafaka za kukabiliana nazo. “Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto halisi inayotugusa sote. Kupitia elimu na utafiti, tunaweza kuchangia suluhisho endelevu kwa mustakabali wa mazingira yetu. Ninawasihi wanafunzi kuchukua jukumu la kuwa mabalozi wa mazingira kwa kuhamasisha juhudi za kulinda mazingira,” alisema Dkt. Ndunguru. Kwa upande wake, Bw. Stephen Mwakabonga, mmoja wa wawezeshaji, alieleza kwa kina maana ya mabadiliko ya tabianchi, vyanzo vyake, na athari zake kwa jamii na uchumi. Alibainisha kuwa shughuli za kibinadamu kama ukataji miti, matumizi ya nishati ya kisukuku, na uchafuzi wa mazingira ni miongoni mwa sababu zinazoathiri hali ya hewa na kusababisha mabadiliko makubwa ya tabianchi. Naye Mhandisi Grace Msangi, ambaye pia ni mwezeshaji wa mhadhara huo, alifafanua kuhusu suluhisho mbalimbali za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Alisisitiza matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, mbinu za kilimo endelevu, na umuhimu wa sera zinazowiana na ulinzi wa mazingira. Kwa upande wake, Bw. Emmanuely Zephaline, alizungumzia matumizi ya mifumo ya ramani za kidigitali na picha za satelaiti katika usimamizi wa mazingira. Warsha hii imeacha alama kwa washiriki, huku wengi wakiahidi kutumia maarifa waliyojifunza ili kuchangia katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa njia endelevu.