Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Kitivo cha Sayansi za Jamii kimeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuendana na mageuzi ya teknolojia ya elimu kwa kuandaa mafunzo ya matumizi ya mfumo wa e-learning kwa wanataaluma wake, yaliyofanyika leo, tarehe 02 Mei 2026, Ukumbi wa Mikutano, Kampasi Kuu Morogoro. Mafunzo hayo yamelenga kuimarisha matumizi ya mifumo ya ujifunzaji mtandaoni na kuongeza ufanisi wa ufundishaji unaoendana na mabadiliko ya teknolojia ya elimu duniani. Ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa chuo wa kukuza uwezo wa wahadhiri katika nyanja za kidijitali. Akifungua mafunzo hayo, Mtiva wa Kitivo cha Sayansi za Jamii, Prof. Harold Utouh alisisitiza umuhimu wa watumishi kujituma katika kujifunza na kutumia maarifa mapya wanayoyapata, akibainisha kuwa mafunzo hayo yamepangwa kwa kuzingatia vipaumbele vya kitivo. Alieleza kuwa kila mhadhiri anapaswa kuwa na utamaduni wa kujitathmini na kujipangia maendeleo yake kitaaluma kwa kutumia fursa zilizopo ndani ya chuo. “Ni muhimu tukatambua kuwa mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa chuo. Hatuwezi kubaki nyuma wakati dunia inaenda mbele kiteknolojia. Lazima tuhakikishe mifumo kama e-learning inatumika kikamilifu katika ufundishaji wetu,” alisema Prof. Utouh. Aidha, Prof. Utouh aliwataka washiriki kuweka mkazo katika vitendo baada ya mafunzo, akieleza kuwa mazoezi ya mara kwa mara ndiyo yatakayowawezesha kumudu matumizi ya mifumo hiyo kwa ufanisi. Aliongeza kuwa kutotumia ipasavyo rasilimali zilizopo kunaweza kuleta uwajibikaji kwa viongozi wa idara na programu, akisisitiza nidhamu ya kazi na uwajibikaji wa pamoja. Katika hatua nyingine, Prof. Utouh aligusia umuhimu wa uanagenzi kwa wahadhiri chipukizi, akieleza kuwa wahadhiri waandamizi wanapaswa kushirikiana na vijana kwa kuwajengea uwezo na kuhamasisha tafiti za pamoja. Alisisitiza pia umuhimu wa kuanzisha na kuhuisha vikundi vya tafiti (research groups) vitakavyosaidia kuongeza machapisho ya kitaaluma na utafutaji wa miradi ya utafiti yenye ufadhili. Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Umahiri katika Ufundishaji na Ujifunzaji wa Kibunifu, Dkt. Perpetua Kalimasi aliwasilisha taarifa ya matumizi ya e-learning katika kitivo hicho, akionesha mafanikio yaliyopatikana pamoja na maeneo yanayohitaji kuboreshwa. Vilevile alitoa muhtasari wa mafunzo hayo, akifafanua kuwa yamelenga kuwajengea washiriki uelewa mpana wa matumizi ya teknolojia katika utoaji wa elimu bora. Nao wawezeshaji wa mafunzo hayo, Bw. Abuu Mshamu na Bi. Halima Rajabu waliendesha vipindi vya kitaalamu vilivyojikita katika mapitio ya mifumo msingi ya e-learning, vipengele na uwezo wake, pamoja na utangulizi wa matumizi ya zana ya H5P katika uundaji wa maudhui shirikishi ya kujifunzia. Washiriki walipata pia fursa ya kufanya mazoezi kwa katika kuunda shughuli mbalimbali za H5P. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika utoaji wa elimu chuoni hapo, huku yakiongeza uwezo wa wahadhiri kutumia kikamilifu mifumo ya e-learning na hivyo kuboresha uzoefu wa ujifunzaji kwa wanafunzi katika zama za kidijitali.