News-Details

News >Details

BW. SIMON AUGUSTINE ANG’ARA KATIKA UTETEZI WA TASNIIFU YA UZAMIVU MZUMBE

BW. SIMON AUGUSTINE ANG’ARA KATIKA UTETEZI WA TASNIIFU YA UZAMIVU MZUMBE

Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kuthibitisha nafasi yake kama kitovu cha tafiti zenye mchango kwa maendeleo ya taifa, kufuatia mwanafunzi wake wa Shahada ya Uzamivu (PhD), Bw. Simon Augustine, kuwasilisha na kutetea tasnifu yake kwa mafanikio makubwa mbele ya jopo la watahini leo tarehe 6 Mei, 2026, katika Ukumbi wa Mihadhara wa Bomani, Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu - Morogoro. Utetezi huo uliongozwa na Mwenyekiti wa jopo la watahini, Prof. Leonada Mwagike, ambapo Bw. Simon aliwasilisha utafiti wake wenye mada isemayo: “Vigezo vinavyoathiri uasili, matumizi na mafanikio ya teknolojia ya mifumo ya taarifa za usimamizi wa miradi katika mashirika ya kiraia nchini Tanzania.” Utafiti huo ulilenga kuchunguza kwa kina sababu zinazoathiri namna mashirika hayo yanavyopokea na kutumia teknolojia za kisasa katika kusimamia miradi yao. Akiwasilisha hoja zake, Bw. Simon alibainisha kuwa licha ya umuhimu mkubwa wa mifumo ya taarifa za usimamizi wa miradi, bado mashirika mengi yanakumbwa na changamoto zinazozuia matumizi yake kwa ufanisi. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na miundombinu duni ya TEHAMA, uelewa mdogo wa watumiaji, pamoja na mapungufu katika sera na mifumo ya usimamizi. Hata hivyo, alisisitiza kuwa kwa uwekezaji sahihi katika maeneo hayo, teknolojia hizo zina uwezo mkubwa wa kuongeza uwazi, ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi. Tasnifu hiyo ilisimamiwa na Prof. Robert Makorere kama msimamizi mkuu, akishirikiana na Prof. Gabriel Komba kama msimamizi msaidizi, ambao walimhudumia mtafiti kwa karibu katika safari yake ya kitaaluma hadi kufikia hatua hiyo muhimu. Baada ya mjadala wa kina, Mwenyekiti wa jopo la watahini, Prof. Mwagike, alimpongeza Bw. Simon kwa umahiri wake wa kitaaluma, akieleza kuwa ameonesha uwezo mkubwa wa kuchambua hoja, kujenga mjadala wenye mashiko na kujibu maswali kwa ufasaha. Aliongeza kuwa utafiti huo una mchango mkubwa katika kuboresha matumizi ya teknolojia za usimamizi wa miradi nchini, hususan katika mashirika ya kiraia. Mafanikio haya si tu ushindi binafsi kwa Bw. Simon Augustine, bali pia ni kielelezo cha ubora wa taaluma unaotolewa na Chuo Kikuu Mzumbe. Ni ushahidi kuwa chuo hicho kinaendelea kuzalisha watafiti na wataalamu wenye uwezo wa kutoa suluhisho bunifu kwa changamoto za maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None