News-Details

News >Details

CHUO KIKUU MZUMBE CHAWAJENGEA UWEZO WAANDISHI CHIPUKIZI KATIKA MATUMIZI YA KISWAHILI SANIFU NA FASAHA

CHUO KIKUU MZUMBE CHAWAJENGEA UWEZO WAANDISHI CHIPUKIZI KATIKA MATUMIZI YA KISWAHILI SANIFU NA FASAHA

Katika jitihada za kuimarisha ubora wa lugha katika tasnia ya habari nchini, Chuo Kikuu Mzumbe kimetoa mafunzo maalum ya Kiswahili sanifu na fasaha kwa wanafunzi wa Chuo cha Uandishi wa Habari Morogoro, hatua inayolenga kuziba pengo la makosa ya lugha yanayojitokeza mara kwa mara katika vyombo vya habari. Mafunzo hayo yamefanyika Mei 05, 2026, mkoani Morogoro, yakihusisha wataalamu wa lugha kutoka Kitivo cha Sayansi za Jamii, hususan Idara ya Lugha na Stadi za Mawasiliano ya Chuo Kikuu Mzumbe, ambapo yaliendeshwa na wataalamu watatu ambao ni Dkt. Issaya Lupogo, Bw. Davian Buguna na Bw. Wenslaus Lugenge, waliotumia mbinu shirikishi kuhakikisha washiriki wanapata uelewa wa kina wa mada zilizowasilishwa. Akifungua rasmi mafunzo hayo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Dkt. Issaya Lupogo alieleza kuwa utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu Mzumbe umebaini uwepo wa changamoto kubwa katika matumizi ya Kiswahili miongoni mwa waandishi wa habari, hali inayoweza kuathiri ubora na uaminifu wa taarifa zinazowasilishwa kwa umma. “Mafunzo haya ni sehemu ya jukumu letu la kitaaluma na kijamii kuhakikisha tunazalisha waandishi wa habari wenye weledi wa hali ya juu katika matumizi ya Kiswahili,” alisema Dkt. Lupogo, huku akiwahimiza washiriki kutumia maarifa hayo kama nyenzo ya kujitofautisha katika soko la ajira. Katika mafunzo hayo, washiriki walipatiwa uelewa mpana kuhusu makosa yaliyozoeleka katika uandishi wa Kiswahili, ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya maneno kama “kwanini” badala ya “kwa nini”, “dharula” badala ya “dharura”, na “maaskari” badala ya “askari”. Aidha, walijifunza tofauti kati ya makosa na dosari katika uandishi, pamoja na namna ya kuboresha mtiririko na uwasilishaji wa habari. Sambamba na hilo, mada kuhusu Mwongozo wa Uandishi wa Nyaraka za Serikali ilitolewa, ambapo washiriki walipatiwa maarifa ya kitaalamu juu ya uandishi sahihi wa barua, kumbukumbu za vikao na nyaraka nyingine rasmi. Msisitizo uliwekwa katika matumizi sahihi ya vifupisho vya “Kuh:” na “Yah:” kulingana na muktadha wa mawasiliano. Kwa upande wao, wanafunzi walieleza kuwa mafunzo hayo yamewapa mwanga mpya katika taaluma yao na kuwaongezea kujiamini katika uandishi wa habari kwa Kiswahili sanifu. Uongozi wa Chuo cha Uandishi wa Habari Morogoro pia ulipongeza hatua hiyo, ukieleza kuwa ni mfano bora wa ushirikiano wa taasisi za elimu ya juu katika kukuza taaluma nchini. Hatua hii ya Mzumbe si tu inaimarisha taaluma ya uandishi wa habari, bali pia inalinda na kukuza matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili kama nyenzo muhimu ya mawasiliano na utamaduni wa Taifa.

None
None
None
None