News-Details

News >Details

KAMBI YA UJASIRIAMALI MZUMBE YACHOCHEA MAWAZO YA KIBUNIFU NA AJIRA KWA VIJANA

KAMBI YA UJASIRIAMALI MZUMBE YACHOCHEA MAWAZO YA KIBUNIFU NA AJIRA KWA VIJANA

Maadhimisho ya Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali yameendelea kwa mafanikio katika Kampasi Kuu Morogoro, ambapo leo tarehe 7 Mei 2026 wadau mbalimbali wakiwemo wanafunzi, wafanyakazi waendeshaji, wanataaluma pamoja na wageni kutoka maeneo mbalimbali wameendelea kushiriki shughuli za kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujionea bunifu mbalimbali zinazowasilishwa chuoni hapo. Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mgeni Rasmi, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Allen Mushi, alisisitiza umuhimu wa ubunifu katika kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana. Alieleza kuwa Chuo kitaendelea kuboresha mitaala na kuimarisha Kituo cha Ubunifu na Uatamiaji wa Miradi (Innovation and Incubation Hub) ili kuwawezesha wanafunzi kukuza na kuendeleza mawazo yao ya kiubunifu kuwa miradi yenye tija. Kwa upande wake, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Taaluma, Utafiti na Ushauri, Profesa Idda Lyatonga Swai, alihimiza wanafunzi kutumia jukwaa hilo kama fursa ya kujifunza kwa vitendo na kubadilishana uzoefu, ili kuimarisha uelewa wao kuhusu ubunifu na ujasiriamali kama nguzo muhimu za maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla. Aidha, Mgeni Maalumu ambaye ni Msajili wa Vyama vya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, alieleza umuhimu wa mfumo wa ushirika katika kuwawezesha vijana na jamii kwa ujumla kushiriki katika shughuli za kiuchumi kwa pamoja. Dkt. Ndiege alibainisha kuwa ushirika ni nyenzo muhimu ya kuongeza tija, kujenga nguvu ya pamoja na kupanua fursa za kiuchumi, hususan kwa vijana wanaoingia katika shughuli za ujasiriamali. Pia, alihimiza umuhimu wa kuimarishwa kwa elimu ya ushirika ili wananchi waweze kunufaika kikamilifu na fursa zilizopo. Naye Meneja wa Ubunifu, Ujasiriamali na Mahusiano ya kitasnia, Profesa Emmanuel Chao, alibainisha kuwa ujuzi na ubunifu ni mtaji muhimu katika soko la ajira la sasa, akihimiza wanafunzi kutumia fursa zilizopo kukuza na kuendeleza vipaji vyao kuwa miradi yenye tija na endelevu. Vilevile, wadau mbalimbali walishiriki mjadala katika jopo kuhusu ubunifu na ujasiriamali, ambapo walijadili nafasi ya ubunifu katika kuchochea ajira na maendeleo ya kiuchumi. Aidha, wanafunzi walipata fursa ya kuonesha ubunifu wao wa mambo mbalimbali kupitia mashindano, ambapo mwanafunzi kutoka Kitivo cha Sayansi na Teknolojia (FST) Bw. Festo John alitangazwa kuwa mshindi kutokana na ubunifu wa mfumo wa kidijitali ulioupa jina la "Mzumbe Student App" unaowezesha upatikanaji wa notisi, mitihani ya zamani (past papers), huduma ya chakula na huduma nyingine za Chuo. Maadhimisho haya yaliyopambwa na kaulimbiu: “Kuwawezesha wajasiriamali wa baadaye kupitia ubunifu, ujuzi na ushirikiano wa kimkakati,” yalianza rasmi tarehe 6 Mei 2026 na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 8 Mei 2026.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None