Maadhimisho ya Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali yaliyodumu kwa siku tatu yametamatishwa rasmi leo tarehe 8 Mei 2026 katika Kampasi Kuu Morogoro. Maadhimisho hayo yaliyoongozwa na kaulimbiu: “Kuwawezesha wajasiriamali wa baadaye kupitia ubunifu, ujuzi na ushirikiano wa kimkakati,” yametoa fursa ya watu kuonesha na kujifunza ubunifu wa masuala mbalimbali na kupata elimu kupitia mawasilisho ya mada mbalimbali. Akizungumza katika hafla ya kufunga maadhimisho hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Aristides Mbwasi, alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za elimu ya juu pamoja na wadau mbalimbali katika kukuza ubunifu na ujasiriamali kwa vijana. Alieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha uchumi shindani na kuongeza fursa za ajira kupitia bunifu zinazozalishwa na vijana nchini. Aidha, Mbwasi alizitaka taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo, ikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), kuendelea kuwa karibu na vijana wabunifu ili kuwasaidia kurasimisha biashara zao na kuendeleza bunifu zao hadi kufikia hatua ya kibiashara kamili. Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Allen Mushi, alieleza kuwa Chuo kimeendelea kuimarisha mazingira ya ubunifu kupitia Kituo cha Ubunifu na Uatamiaji wa Miradi, ambacho kimefanikisha kusaidia kuanzishwa kwa zaidi ya makampuni 100 yanayofanya shughuli zake ndani na nje ya nchi. Alisema mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za chuo katika kuwajengea wanafunzi uwezo wa kubadilisha maarifa ya darasani kuwa miradi halisi yenye mchango katika ajira na maendeleo ya kiuchumi. Naye Meneja wa Ubunifu, Ujasiriamali na Mahusiano ya Kitasnia, Profesa Emmanuel Chao, alieleza kuwa Chuo kinaendelea kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za fedha na wadau wa maendeleo ili kuwawezesha vijana kuendeleza biashara endelevu na zenye ushindani katika soko. Aliongeza kuwa kumekuwepo ongezeko la wakurugenzi wa makampuni mbalimbali yaliyoanzishwa na wahitimu pamoja na fursa nyingi za ajira zinazowawezesha vijana kujiajiri na kuajiri wengine. Akifunga rasmi maadhimisho hayo, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Taaluma, Utafiti na Ushauri, Profesa Idda Lyatonga Swai, alieleza kuwa maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kukuza ubunifu na ujasiriamali miongoni mwa vijana. Alisisitiza kuwa Chuo kitaendelea kuimarisha mifumo ya mafunzo ya vitendo ili kuhakikisha wanafunzi wanabadilisha maarifa yao kuwa suluhisho halisi la changamoto za kijamii na kiuchumi. Mwisho, Prof. Idda aliwashukuru na kuwapongeza wote walioshiriki siku tatu za maadhimisho ya Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali na kuwaomba kuyafanyia kazi maarifa waliyoyapata.