Huzuni na simanzi vimetanda katika Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu Morogoro, kufuatia vifo vya wanafunzi wawili vilivyotokea tarehe 6 Mei 2026. Jumuiya ya chuo Kikuu Mzumbe, ilikusanyika kwa pamoja kushiriki ibada ya kuwaaga marehemu na kutoa heshima za mwisho, ambapo wanafunzi na watumishi walijumuika kuomboleza pamoja huku wakikumbuka maisha na mchango wa marehemu wakati wa uhai wao chuoni hapo. Marehemu, Bi. Witness Samora Samila, mwanafunzi wa mwaka wa pili aliyekuwa akisoma Shahada ya Awali ya Uhasibu na Fedha katika Sekta ya Umma, aliyefariki kutokana na mshtuko wa moyo akiwa chuoni hapo. Naye Bi. Nyabatende B. Julias, mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Shahada ya Awali ya Usimamizi wa Rasilimali Watu, aliyefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro alipokuwa akipatiwa matibabu. Ibada hiyo ya kuaga na kuwaombea marehemu ilihudhuriwa na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Allen Mushi, ambaye alitoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu pamoja na jumuiya nzima ya chuo. Alisisitiza umuhimu wa mshikamano, upendo na kusaidiana katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. Baada ya ibada hiyo, miili ya marehemu iliagwa rasmi huku waombolezaji wakitoa heshima zao za mwisho katika hali ya utulivu na huzuni kubwa. Tukio hilo limeacha pengo kubwa chuoni hapo, huku kumbukumbu za marehemu zikiendelea kubaki mioyoni mwa wanafunzi wa chuo hicho.