Chuo Kikuu Mzumbe kimeshiriki Mkutano Mkuu wa Pili Jumuishi wa Mwaka wa Jumuiya za Wataalamu wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma Tanzania 2026 uliofanyika jijini Arusha kuanzia Mei 5 hadi 8, 2026, ukiwakutanisha wataalamu wa utawala, rasilimali watu na viongozi wa taasisi mbalimbali za umma kujadili maendeleo ya utumishi wa umma na mbinu za kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Ujumbe wa Chuo Kikuu Mzumbe uliongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu, Bi. Sophia Mchomvu, akiwa ameambatana na Maafisa Utawala pamoja na Maafisa Rasilimali Watu kutoka kurugenzi hiyo. Ushiriki wa Mzumbe katika mkutano huo umeendelea kutoa fursa kwa watumishi wake kupata uzoefu wa kitaaluma, kujifunza mifumo mipya ya usimamizi wa rasilimali watu na kuimarisha mahusiano ya kitaaluma na taasisi nyingine za umma. Katika mkutano huo, washiriki walijadili masuala mbalimbali ikiwemo matumizi ya teknolojia katika utumishi wa umma, maadili ya kazi, uongozi na usimamizi wa watumishi pamoja na mbinu za kuongeza uwajibikaji na tija katika taasisi za umma. Mjadala mkubwa pia ulijikita katika namna taasisi zinavyoweza kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidijitali ili kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma. Akifungua mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, aliwahimiza wataalamu wa utawala na rasilimali watu kutumia taaluma zao kuleta mageuzi chanya katika utumishi wa umma kwa kuzingatia uwajibikaji, ubunifu na maadili ya kazi. Ushiriki wa Chuo Kikuu Mzumbe katika mkutano huo unaendelea kuimarisha juhudi za Chuo katika kukuza uwezo wa watumishi wake na kuboresha mifumo ya utawala na usimamizi wa rasilimali watu kwa ajili ya kuongeza ubora wa huduma ndani ya taasisi.