Semina ya kuwasilisha matokeo ya awali ya utafiti wa sayansi ya jamii kuhusu mabadiliko ya tabianchi na maji imefanyika tarehe 30, Aprili 2026 katika Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro, ikiwa ni sehemu ya mradi wa ICP Connect na Lab to Life, wa awamu ya pili ya mradi huo kuanzia mwaka 2022 hadi 2027, unaotekelezwa kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Antwerp (Ubelgiji), Chuo Kikuu Mzumbe, Taasisi ya Sera ya Maendeleo (IOB), Chuo Kikuu cha Kikristo cha Uganda (UCU) na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika ya Nelson Mandela (NM-AIST Arusha). Semina hiyo imewakutanisha waratibu wa miradi, wageni waalikwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Bodi ya Maji ya Bonde la Wami/Ruvu, TURUWASA Mvomero, pamoja na viongozi wa kata na vijiji kutoka Tarafa ya Turiani, watafiti, wanafunzi na wafanyakazi wa kitaaluma kutoka taasisi washirika. Akifungua semina hiyo, akimwakilisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma, Utafiti na Ushauri), Dkt. Proscovia Kamugisha alisema kuwa mradi huo umeongeza uwezo wa kitaifa katika ufuatiliaji na tathmini kupitia Shahada ya Uzamili ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Maendeleo (MDME), akisisitiza kuwa lengo la semina ni kushirikisha matokeo ya awali ya tafiti na kuimarisha ushirikiano kati ya utafiti, jamii na watunga sera. Kwa upande wake, Mratibu wa mradi, Dkt. Christina Shitima alieleza kuwa mradi umeimarisha ushirikiano kati ya chuo na jamii kwa kuwashirikisha wananchi moja kwa moja katika tafiti, hatua inayoongeza uelewa wa pamoja na ushirikiano endelevu katika kushughulikia changamoto za mabadiliko ya tabianchi na maji. Naye Dkt. Lucy Massoi alieleza kuwa ushirikishwaji wa wadau unafanya jamii kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zao, jambo linalosaidia kuboresha sera na maisha ya kila siku. Akichangia katika semina hiyo, Bw. Richard Temu kutoka shirika la Twaweza alieleza kuwa mbinu za uraghibishaji (animation) zina mchango mkubwa katika kuwabadilisha wananchi kutoka kuwa wasikilizaji wa taarifa pekee na kuwafanya kuwa washiriki hai katika mchakato wa kutambua, kuchambua na kutatua changamoto zinazowakabili. Alisisitiza kuwa mbinu hizo huimarisha uelewa wa pamoja kati ya watafiti na jamii, jambo linalochochea ushiriki wa kweli na ufumbuzi endelevu wa matatizo ya kijamii. Katika uwasilishaji wa tafiti, wanafunzi walieleza mafanikio yao katika kijiji cha Kilimanjaro, Kisala, Turiani Wilayani Mvomero, ambapo waliweka kifaa cha ufuatiliaji wa hali ya hewa kinachopima kasi ya upepo, unyevunyevu na mwenendo wa maji mtoni. Takwimu hizo husaidia kutoa tahadhari ya mapema kuhusu mafuriko na kuimarisha maandalizi ya jamii dhidi ya majanga ya asili. Kundi jingine la wanafunzi katika utafiti uliofanyika katika kijiji cha Lusanga lilibainisha changamoto za maji zikiwemo vyanzo visivyo salama, upungufu wa maji wakati wa kiangazi, changamoto za miundombinu na ukosefu wa mpango endelevu wa huduma za maji. Walipendekeza kuimarishwa kwa ushiriki wa jamii katika usimamizi wa maji, ulipaji wa ada kwa wakati, pamoja na matumizi ya mbinu rahisi za usafi kama kuyachemsha au kuyachuja maji, sambamba na kuimarisha uhifadhi salama wa maji. Semina hiyo ilifungwa na Dkt. Robert Lihawa, Kaimu Mkuu wa Idara ya Uchumi kutoka Kitivo cha Sayansi ya Jamii, ambaye alisema kuwa tafiti shirikishi ni muhimu katika kuunganisha jamii, watafiti na watunga sera kwa maendeleo endelevu.