News-Details

News >Details

CHUO KIKUU MZUMBE CHASHIRIKI MAADHIMISHO YA MEI MOSI MKOANI MOROGORO

CHUO KIKUU MZUMBE CHASHIRIKI MAADHIMISHO YA MEI MOSI MKOANI MOROGORO

Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) kutoka Chuo Kikuu Mzumbe wameungana na wafanyakazi wengine kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) mwaka 2026, yaliyofanyika wilayani Gairo, mkoani Morogoro, tarehe 1 Mei 2026. Maadhimisho hayo yameongozwa na kaulimbiu isemayo “Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050,” ikilenga kuhamasisha wafanyakazi kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na kuzingatia maadili ya kazi. Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kigoma Malima, aliwapongeza wafanyakazi wa Mkoa wa Morogoro kwa mshikamano na ushirikiano waliouonesha wakati wa maandamano na shughuli za siku hiyo. Amesema kuwa umoja huo ni kielelezo cha kutambua umuhimu wa kazi kama nyenzo ya kufikia mafanikio ya pamoja, huku akisisitiza kuwa wafanyakazi ni rasilimali muhimu ya kimkakati katika kufanikisha maendeleo endelevu ya taifa. Mhe. Malima alieleza kuwa Serikali, kwa kushirikiana na vyama vya wafanyakazi, imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha maslahi ya watumishi, ikiwemo kupandisha vyeo, kufanya marekebisho ya madaraja na kuongeza mishahara. Aidha, aliwataka wafanyakazi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu ili kuchangia kikamilifu utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Bw. Elias Mtungilwa, amewahimiza wafanyakazi kote nchini kuzingatia uwiano kati ya haki na wajibu, akibainisha kuwa hakuna haki bila utekelezaji wa majukumu. Amesisitiza umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na miongozo iliyopo pamoja na kuendeleza ubunifu ili kuongeza tija na ufanisi kazini. Aidha, akitoa risala kwa Mgeni Rasmi, Mratibu wa Siku ya Mei Mosi Mkoa wa Morogoro, Bw. Alphonce Mbasa, ameeleza changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi, ikiwemo ucheleweshaji wa nyongeza za mishahara, maslahi duni pamoja na malimbikizo ya madai ya watumishi. Ameitaka Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa kuzingatia hali halisi ya maisha ya wafanyakazi na kufanya tafiti zitakazosaidia kupanga viwango stahiki vya mishahara. Maadhimisho hayo yameimarisha mshikamano miongoni mwa wafanyakazi wa sekta za umma na binafsi mkoani Morogoro, huku yakisisitiza umuhimu wa kazi zenye staha, uwajibikaji na ushirikiano katika kufikia maendeleo endelevu. Ushiriki wa Chuo Kikuu Mzumbe umeendelea kudhihirisha dhamira ya taasisi hiyo katika kuunga mkono juhudi za kitaifa za kukuza tija kazini na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

None
None
None
None
None
None
None
None
None