Chuo Kikuu Mzumbe, kupitia Kitengo cha Mafunzo Mafupi, Ubunifu, Ushauri na Huduma kwa Jamii (Short Courses, Innovations, Consultancy and Outreach Services Unit) cha Ndaki ya Dar es Salaam, kimeendesha mhadhara wa wazi uliolenga kuunganisha nadharia na vitendo katika usimamizi wa huduma za kijamii na kiuchumi nchini Tanzania. Mhadhara huo umefanyika tarehe 4 Mei 2026 katika Kituo cha Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi ya Dar es Salaam-Tegeta. Mhadhara huo uliwasilishwa kwa mada isemayo “Kuunganisha Nadharia na Vitendo: Mtazamo wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Usimamizi wa Huduma za Kijamii na Kiuchumi nchini Tanzania”, ukilenga kutoa uelewa wa kina kuhusu mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuboresha huduma kwa jamii na kukuza maendeleo ya kiuchumi. Akiwasilisha mada hiyo, Mkurugenzi Mtendaji CR Hope Foundation, Bw. Augustine Mwombeki, alieleza kwa kina namna mashirika yasiyo ya kiserikali yanavyoweza kuunganisha nadharia na utekelezaji wa vitendo katika utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi. Alisisitiza umuhimu wa kutumia uzoefu wa vitendo pamoja na maarifa ya kitaaluma katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii. Akifafanua zaidi, Bw. Mwombeki alibainisha kuwa ushirikiano kati ya wadau mbalimbali, ubunifu katika utekelezaji wa miradi, pamoja na matumizi sahihi ya rasilimali ni mambo muhimu yanayoweza kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma. Aidha, alieleza kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali yana nafasi kubwa katika kusaidia juhudi za serikali kufikia maendeleo endelevu. Kwa upande wao, washiriki wa mhadhara huo walipata fursa ya kuuliza maswali na kuchangia hoja mbalimbali, hali iliyosaidia kuongeza uelewa na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bora za kusimamia huduma za kijamii na kiuchumi. Akishukuru kwa niaba ya wanafunzi wenzake, mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya Utawala wa Umma, Bw. Yohana Nicholous, alilishukuru shirika hilo kwa kutoa fursa ya mhadhara huo na kuwaomba kuwa pale inapojitokeza fursa nyingine zisite kuendelea kushirikiana na wanafunzi kwa kuwapatia mafunzo na uzoefu zaidi wa vitendo. Mhadhara huo ni sehemu ya juhudi za Chuo Kikuu Mzumbe katika kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya taaluma na utekelezaji wa vitendo, pamoja na kutoa jukwaa la kujifunza na kubadilishana maarifa kati ya wataalamu, wanafunzi na wadau wa maendeleo.