Katika jitihada za kuwaandaa wanafunzi kuwa wabunifu, waajiriwa na waajiri wenye uwezo wa kushindana katika soko la ajira, Chuo Kikuu Mzumbe kimeendesha mhadhara wa umma uliowakutanisha wanafunzi, ukihusisha mada mbalimbali zikiwemo ujasiriamali, ubunifu, utambuzi na uundaji wa fursa, stadi za maisha pamoja na elimu ya miliki bunifu. Mhadhara huo ulifanyika tarehe 6 Mei 2026 katika Kampasi Kuu, Morogoro. Akizungumza katika mhadhara huo, Mwezeshaji wa mada ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Sokoine University Graduate Entrepreneurs Cooperative (SUGEC), Bw. Joseph Masimba, aliwasilisha mada kuhusu mabadiliko ya kimtazamo, utambuzi wa fursa na uanzishaji wa biashara. Alisisitiza umuhimu wa wanafunzi kubadili mtazamo na kujenga fikra za kiuajasiriamali, pamoja na kujitengenezea thamani binafsi inayoweza kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kuvutia uwekezaji. Kwa upande wake, Meneja wa Uchangishaji Fedha na Ushirikiano kutoka shirika la ANZA Entrepreneurs, Bi. Angelah Rutta, aliwasilisha mada kuhusu upatikanaji na uundaji wa fursa kwa vijana. Alieleza kuwa fursa haziji zenyewe bali zinahitaji juhudi za makusudi, ikiwemo kujenga mitandao, kuimarisha ushirikiano na kutumia ubunifu katika kuzitambua na kuziendeleza. Aidha, Afisa Mtendaji Mkuu wa Acceleration of Life Skill Foundation (ALSF), Bw. Thomas Mchiwa, aliwasilisha mada kuhusu stadi za maisha, akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, nidhamu na juhudi binafsi katika kufikia mafanikio ya kitaaluma na kijamii. Alibainisha kuwa mafanikio yanahitaji uvumilivu, kujituma na uwezo wa kukamilisha malengo yaliyoanzishwa. Katika kuongeza uelewa wa kisheria na kiuchumi, Msajili Msaidizi kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bi. Neema Kitala, aliwasilisha mada kuhusu elimu ya miliki bunifu. Alifafanua umuhimu wa kulinda ubunifu kupitia usajili wa biashara, makampuni na alama za biashara, hatua inayochangia kuongeza ushindani na kuimarisha utambulisho wa bidhaa na huduma sokoni. Mhadhara huo umechangia kuwajengea wanafunzi uelewa mpana kuhusu mbinu za kujiajiri, umuhimu wa ubunifu na matumizi sahihi ya fursa zilizopo, pamoja na kuwapa maarifa ya msingi ya kisheria katika kuanzisha na kuendesha biashara. Hatua hii inatarajiwa kuongeza ari ya ujasiriamali miongoni mwa wanafunzi na kuwawezesha kujitegemea pamoja na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.