News-Details

News >Details

PROF. MWEGOHA AITAKA JAMII YA MZUMBE KUSHIRIKI MICHEZO ILI KUKUZA VIPAJI NA KUIMARISHA AFYA

PROF. MWEGOHA AITAKA JAMII YA MZUMBE KUSHIRIKI MICHEZO ILI KUKUZA VIPAJI NA KUIMARISHA AFYA

Michezo imeelezwa kuwa nyenzo muhimu katika kukuza vipaji vya vijana, kuimarisha afya pamoja na kujenga mshikamano miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu, huku menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe ikiahidi kuendelea kuwekeza zaidi katika maendeleo ya michezo na miundombinu yake. Hayo yameelezwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, wakati akifungua rasmi Mashindano ya Michezo ya Vitivo 2026 yaliyofanyika tarehe 16 Mei 2026 katika Viwanja vya Michezo vya Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu Morogoro. Mashindano ya Michezo ya Vitivo 2026 yamefanyika kwa uratibu wa Menejimenti ya Chuo na udhamini wa Tuzo za wachezaji bora uliofanywa na Ilula Orphans Program, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za maendeleo ya michezo na vipaji vya vijana chuoni hapo. Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Mwegoha alisema michezo imeendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha ya wanafunzi kwani huwasaidia kujenga afya bora, kuibua vipaji na kuongeza ushirikiano na mahusiano miongoni mwao. Amesema kupitia mashindano hayo, wanafunzi wanapata nafasi ya kujifunza ushindani wa kirafiki, nidhamu pamoja na kujenga mtandao wa kijamii unaoweza kuwasaidia hata baada ya maisha ya chuo. “Michezo ina faida kubwa sana kwa vijana wetu. Mbali na kukuza vipaji, pia ni sehemu ya kujenga afya na kuimarisha mshikamano. Kupitia michezo wanafunzi wanapata nafasi ya kushirikiana, kujifunza na hata kujitangaza vipaji vyao,” amesema Prof. Mwegoha. Aidha, Prof. Mwegoha amepongeza kamati ya maandalizi, viongozi wa michezo pamoja na wanamichezo kwa kufanikisha maandalizi ya mashindano hayo. Pia amesema menejimenti ya chuo itaendelea kuboresha mazingira ya michezo chuoni hapo ikiwemo miundombinu ya viwanja, maeneo ya huduma muhimu kama vyoo na mabafu pamoja na mifumo ya maji na drainage ili kuhakikisha mazingira bora kwa wanamichezo na watazamaji. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi Chuo Kikuu Mzumbe, Alphonce Kauky, amepongeza juhudi za kamati ya maandalizi pamoja na wanafunzi walioshiriki mashindano hayo huku akisisitiza umuhimu wa michezo katika kujenga afya, nidhamu na ushiriki wa wanafunzi katika shughuli za kijamii chuoni hapo. Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu Mzumbe, Samuel Chacha, amesema mashindano hayo ni sehemu muhimu ya kuwaunganisha wanafunzi kutoka vitivo mbalimbali kupitia michezo, huku akiwahamasisha wanafunzi kujitokeza kwa wingi kushiriki na kushangilia michezo hiyo kwa amani na mshikamano. Amesema michezo hiyo pia ni jukwaa muhimu la kukuza vipaji vya wanafunzi na kuimarisha mahusiano baina ya vitivo na shule mbalimbali za chuo hicho. Akizungumzia historia ya mashindano hayo, Mkufunzi wa Michezo Chuo Kikuu Mzumbe, Yohana Magongo, amesema Mashindano ya Michezo ya Vitivo tangu mwaka 2010 na mwaka huu zinafanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 25 tangu Mzumbe kupata hadhi ya kuwa chuo kikuu. Bw. Magongo amesema mashindano hayo yanahusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, mpira wa pete, tenisi, tenisi ya mezani, mpira wa fimbo pamoja na riadha kwa wanaume na wanawake. Ameongeza kuwa mashindano hayo yataendelea hadi tarehe 6 Juni 2026 ambapo michezo ya fainali inatarajiwa kufanyika. Mashindano ya Michezo ya Vitivo 2026 yanatarajiwa kuendelea kuvutia ushiriki mkubwa wa wanafunzi huku yakitazamwa kama sehemu muhimu ya kuimarisha afya, vipaji, ushirikiano na utamaduni wa michezo ndani ya Chuo Kikuu Mzumbe.

None
None
None
None
None
None
None
None
None