Watumishi wapya wa Chuo Kikuu Mzumbe wamepatiwa semina elekezi yenye lengo la kuwajengea uelewa kuhusu mfumo wa kazi, maadili ya utumishi wa umma pamoja na taratibu za utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi chuoni hapo. Semina hiyo imefanyika Mei 26, 2026 Kampasi Kuu Morogoro, ikiratibiwa na Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala kupitia Kurugenzi ya Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu. Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, Mkuu wa Kitengo cha Uthibiti Ubora, Dkt. Lawrencia Mushi alisema semina hiyo inalenga kuwapa watumishi wapya uelewa mpana kuhusu mazingira ya kazi, wajibu wao wa kila siku pamoja na miongozo ya Utumishi wa Umma na kanuni za Chuo Kikuu Mzumbe ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuchangia maendeleo ya taasisi na Taifa kwa ujumla. Dkt. Mushi alisisitiza kuwa mtumishi bora anapaswa kuendelea kujifunza na kufahamu taratibu, sheria na kanuni mbalimbali zitakazomwezesha kufanya kazi kwa ufanisi, uwajibikaji na kuzingatia maadili ya kazi. Aidha, aliwataka watumishi hao kutumia taaluma na ubunifu wao kuongeza tija katika utoaji wa huduma chuoni hapo. Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu, Afisa Rasilimali Watu, Bi. Praise Maro alisema mafunzo hayo yameandaliwa kuwasaidia watumishi wapya kuifahamu taasisi, kujenga mshikamano mahali pa kazi na kuwawezesha kuendana na mabadiliko ya kiutendaji katika mazingira ya kisasa ya kazi. Katika semina hiyo, washiriki walipata mada mbalimbali kutoka kwa wataalamu wa Chuo, akiwemo Prof. Jenipher Kasanda Sesabo aliyewasilisha mada kuhusu Uthibiti Ubora, Bw. Alexander Benidicto aliyeeleza matumizi ya mifumo ya TEHAMA ya Serikali inayotumika chuoni, pamoja na Bw. Valentine Mbawala aliyetoa mada kuhusu taratibu za Utumishi wa Umma, kanuni na miongozo ya kazi. Watumishi hao pia walipata fursa ya kufahamishwa kuhusu vyama vya wafanyakazi, mifuko ya faraja na huduma za SACCOS zinazopatikana chuoni, hatua inayolenga kuimarisha mshikamano, ustawi wa wafanyakazi na usalama wa mazingira ya kazi. Kwa upande wao, watumishi wapya waliushukuru uongozi wa Chuo kwa kuandaa mafunzo hayo wakieleza kuwa yamewasaidia kuelewa vizuri muundo wa taasisi, wajibu wao kazini na mipaka ya utumishi wa umma, hali itakayowaongezea ari na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.