Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha leo tarehe 26 Mei 2026 amewataka wanafunzi wa Ndaki ya Dar es Salaam kutumia vyema fursa ya elimu ya juu kwa kujituma katika masomo, kuzingatia nidhamu na kujijengea uwezo wa ushindani. Prof. Mwegoha ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Ndaki ya Dar es Salaam - Kituo cha Tegeta iliyojumuisha kupokea taarifa ya maendeleo ya kituo hicho, kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa jengo la Utawala, maboresho ya maktaba, Chumba cha TEHAMA, viwanja vya michezo, vibwete pamoja na eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, pamoja na kufanya mazungumzo na wanafunzi. Akizungumza na wanafunzi, Prof. Mwegoha alieleza kuwa maisha ya chuo ni hatua muhimu ya mabadiliko kwa vijana wengi, hivyo yanahitaji nidhamu, uwajibikaji na maamuzi sahihi yatakayowasaidia kutimiza ndoto zao za kitaaluma na maisha kwa ujumla. “Msisahau sababu iliyowaleta hapa. Jengeni uwezo wa kushirikiana, kuongoza, kujifunza kutoka kwa wengine na kutumia muda wenu vizuri ili muwe watu wenye mchango mkubwa kwa jamii na taifa,” alisema Prof. Mwegoha. Aidha, aliwahamasisha wanafunzi kushiriki michezo, shughuli za kijamii na uongozi wa wanafunzi huku wakidumisha maadili, nidhamu na bidii katika masomo yao. Kwa upande wake, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Gabriel Komba aliwataka wanafunzi kutumia teknolojia na akili mnemba (AI) kwa manufaa ya kujifunza na kuongeza maarifa badala ya kutegemea teknolojia hizo kufanya kazi zao za kitaaluma bila kuelewa walichojifunza. Pia, Prof. Komba aliwataka wanafunzi kutambua kuwa jukumu lao kubwa chuoni ni kujifunza na kujijenga kitaaluma ili kuendelea kulinda heshima na ubora wa wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe katika soko la ajira. Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi alisema Chuo kinaendelea kuboresha miundombinu ya Kituo cha Tegeta kupitia miradi mbalimbali inayolenga kuimarisha mazingira ya kujifunzia na ustawi wa wanafunzi. Awali, Mkuu wa Ndaki ya Dar es Salaam, Prof. Cyriacus Binamungu aliwahimiza wanafunzi kuongeza juhudi katika masomo yao huku akibainisha kuwa Chuo kinaendelea kuongeza wahadhiri na kuboresha huduma mbalimbali za kitaaluma ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora yenye ushindani ndani na nje ya nchi. Ziara hiyo imeacha ujumbe wa kimkakati unaoimarisha nafasi ya Chuo Kikuu Mzumbe kama chimbuko la ubora na uongozi, huku ikisisitiza kuwa elimu bora ni msingi wa mabadiliko na ushindani wa kweli katika dunia ya sasa.