News-Details

News >Details

CHUO KIKUU MZUMBE CHAWAPATIA MAFUNZO VIONGOZI WA KATA YA MZUMBE KUHUSU MAZINGIRA, JAMII NA UTAWALA BORA

CHUO KIKUU MZUMBE CHAWAPATIA MAFUNZO VIONGOZI WA KATA YA MZUMBE KUHUSU MAZINGIRA, JAMII NA UTAWALA BORA

Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Skuli ya Biashara, Idara ya Uhasibu na Usimamizi wa Fedha, kimetoa mafunzo ya siku moja tarehe 26 Machi 2026 kuhusu matumizi ya misingi ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG) katika kuimarisha maendeleo endelevu ya jamii. Mafunzo hayo yamefanyika katika Kampasi Kuu ya Morogoro, na kuwashirikisha viongozi wa vijiji kutoka Kata ya Mzumbe, huku yakilenga kuwajengea uwezo wa kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo kwa kuzingatia misingi ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora ili kukuza ustawi wa kijamii, kiuchumi na uhifadhi wa mazingira katika maeneo yao. Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Umma wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Bertha Mwinuka, aliwahimiza viongozi hao kutumia maarifa watakayopata kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika jamii zao, akisisitiza kuwa uongozi bora unaozingatia maadili na uwajibikaji ni msingi wa maendeleo endelevu. Naye, Mwezeshaji wa Mafunzo hayo ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Moshi Derefa, alieleza kwa kina namna dhana ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora inavyoweza kutumika kama nyenzo ya kimkakati katika kuimarisha utendaji wa viongozi wa ngazi ya jamii. Alibainisha kuwa, uongozi unaozingatia misingi hiyo una uwezo wa kuleta uwiano kati ya maendeleo ya kiuchumi, ustawi wa jamii na uhifadhi wa mazingira, jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya muda mrefu. _“Msingi wa maendeleo endelevu hauko tu katika miradi, bali katika namna viongozi wanavyofanya maamuzi yanayozingatia mazingira, haki za jamii na misingi ya uwajibikaji. Mazingira, Jamii na Utawala Bora si nadharia, bali ni mwongozo wa vitendo kwa uongozi bora na maendeleo ya kweli ya wananchi”_ alisisitiza Dkt. Derefa. Katika kutambua mchango wa Chuo Kikuu Mzumbe katika mafunzo hayo washiriki mbalimbali walikipongeza Chuo hicho kwa kuandaa mafunzo hayo, ambapo yamewapa uelewa mpya na mbinu bora zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi. Washiriki hao waliongeza kuwa elimu waliyoipata itasaidia kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi, kuongeza uwazi katika maamuzi, na kusimamia vyema rasilimali za mazingira katika maeneo yao, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo endelevu ya jamii.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None