Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Skuli ya Biashara, Idara ya Masoko na Ujasiriamali, kimeendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wajasiriamali katika uandaaji na ukuzaji wa biashara, yenye lengo la kuwajengea washiriki ujuzi wa kubuni, kuanzisha na kukuza biashara, ikiwemo kuongeza vyanzo vya mapato binafsi. Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 10 Aprili 2026 katika Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro, yakihusisha washiriki mbalimbali ambao ni walimu kutoka Shule ya Msingi Mzumbe na Shule ya Sekondari Mzumbe huku wakipokelewa na Wawezeshaji kutoka Chuoni hapo. Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Amidi wa Skuli ya Biashara ambaye pia ni Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Bw. Kibhuli Mwita aliwahimiza washiriki kutumia ipasavyo fursa ya mafunzo hayo kwa kujenga uelewa mpana wa masuala ya ujasiriamali, akisisitiza kuwa ujuzi wa biashara unaweza kuwa nyenzo muhimu ya kujiongezea kipato na kuboresha ustawi wa maisha. Mafunzo hayo yalipambwa na mfululizo wa mawasilisho ya kitaalamu kutoka kwa wawezeshaji wa Chuo Kikuu Mzumbe, yakilenga kuwajengea washiriki uelewa wa kina na ujuzi wa vitendo katika masuala ya biashara. Wasilisho la kwanza lilitolewa na Mhadhiri Msaidizi, Bw. Lwako Lubida, aliyejadili mada ya kuwezesha wajasiriamali kupitia uandaaji na maendeleo ya biashara, akieleza mbinu za kubaini fursa, kupanga mikakati na kuhakikisha uendelevu wa biashara. Wasilisho la pili lilitolewa na Mhadhiri Msaidizi, Bi. Nashtwat Hassani, ambaye alifafanua kwa kina hatua za kuandaa mpango wa biashara, akisisitiza umuhimu wa utafiti wa soko, upangaji wa rasilimali, pamoja na maandalizi ya mpango wa kifedha unaoendana na uhalisia wa mazingira ya biashara. Mafunzo hayo yalihitimishwa na wasilisho la tatu kutoka kwa Mkufunzi Msaidizi, Bw. Ally Mohamedi, aliyeelezea umuhimu wa mitandao ya kibiashara katika kukuza biashara, akibainisha namna ya kujenga mahusiano na wadau, kutumia majukwaa mbalimbali ya kijamii na kitaaluma, pamoja na kuongeza wigo wa masoko na fursa za kibiashara. Akifunga mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Masoko na Ujasiriamali wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Moses Marko alisisitiza umuhimu wa washiriki kuyatumia maarifa waliyoyapata kwa vitendo ili kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi zitakazowaongezea kipato na kuimarisha hali zao za maisha, huku akihimiza kuendeleza ushirikiano na kujifunza mara kwa mara ili kukabiliana na changamoto za soko. Nao washiriki wa mafunzo hayo hawakusita kukishukuru Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuandaa mafunzo hayo yenye tija, wakieleza kuwa yamewapa uelewa mpya na ujasiri wa kuanzisha na kukuza biashara, pamoja na matumaini ya kuboresha kipato chao na maisha kwa ujumla.