News-Details

News >Details

MZUMBE KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI NA UNDP KATIKA KUWEZESHA VIJANA KUKUZA TAFITI NA BUNIFU

MZUMBE KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI NA UNDP KATIKA KUWEZESHA VIJANA KUKUZA TAFITI NA BUNIFU

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amehudhuria katika hafla ya kihistoria ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) baina ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Taasisi za Elimu ya Juu nchini, iliyofanyika leo tarehe 29 Mei 2026 katika Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam. Katika hafla hiyo, Prof. Mwegoha ameshuhudia zaidi ya Taasisi 10 za Elimu ya Juu zikiingia katika ushirikiano wenye lengo la kuleta mageuzi ya kimaendeleo. Ushirikiano huo una lenga kupanua wigo wa fursa na kujenga uwezo katika maeneo mbalimbali ya kipaumbele, ikiwa ni pamoja na kukuza Ubunifu na Ujasiriamali kwa Vijana kwa kuanzisha na kuendeleza vituo vya kuatamia mawazo ya kibiashara (incubation hubs) ili kuwezesha vijana wabunifu vyuoni kukuza mawazo yao kuwa biashara zinazoweza kuajiri na kujiajiri. Ushirikiano mwingine ni katika eneo la Tafiti za pamoja na machapisho yenye tija yanayolenga kutatua changamoto halisi za jamii na kuchangia katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Aidha, ushirikiano huo pia unaangazia mageuzi ya Kidijitali na Teknolojia kwa kubadilishana uzoefu na kushirikiana katika matumizi ya teknolojia mpya, akili mnemba (AI), na mifumo ya kidijitali katika kuboresha ujifunzaji na utendaji kazi wa taasisi sambamba na kujenga uwezo wa kitaaluma na kiutendaji katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi, nishati mbadala na usimamizi wa rasilimali za mazingira. Nyanja nyingine za ushirikiano ni katika taaluma na Sekta Binafsi ili kujenga daraja la kimkakati kati ya vyuo vikuu na sekta ya viwanda katika kuhakikisha mitaala inakidhi soko la ajira la sasa na la baadae. Pia, hafla hiyo ilipambwa na ushuhuda kutoka kwa vijana wanufaika wa programu ya UNDP ya Mabalozi wa Vijana ambao walieleza jinsi programu hiyo ilivyowajengea uwezo wa kiuongozi, ujuzi wa kidijitali, na kuwapa fursa za kimataifa zilizofungua milango ya mafanikio katika nyanja mbalimbali za kitaalamu na kibiashara. Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, alimhakikishia Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kitaendelea kuwa mshirika imara na wa kuaminika. "Chuo Kikuu Mzumbe kipo tayari wakati wote kushirikiana na UNDP katika maeneo yote ya kibobevu. Tumejipanga kikamilifu kuwa sehemu ya kwanza na ya kimkakati katika mipango yote ya UNDP inayolenga kunoa vipaji vya vijana, kuwajengea uwezo na kuwasaidia kufikia ndoto zao ili waweze kuliletea taifa maendeleo endelevu," alisisitiza Prof. Mwegoha. Ushirikiano huu unatajwa na wadau wa elimu kuwa hatua kubwa itakayochochea mageuzi ya kiuchumi na kijamii nchini, huku vyuo vikuu vikitajwa kama injini kuu ya kuzalisha maarifa na ubunifu unaohitajika katika karne ya 21. Ikumbukwe kuwa, Chuo Kikuu Mzumbe ndicho kilikuwa chuo kikuu cha kwanza nchini kuingia katika ushirikiano huu wa kimkakati na UNDP, na hivyo kuweka msingi imara wa ushirikiano kwa taasisi nyingine za kitaaluma.

None
None
None
None
None
None
None