Chuo Kikuu Mzumbe kimeandika historia nyingine ya mafanikio baada ya kuibuka mshindi wa jumla katika Maonesho ya 13 ya Biashara na Utalii ya Tanga, ushindi unaodhihirisha ubora wa huduma zake za elimu, utafiti, ubunifu na mchango wake katika maendeleo ya jamii. Mafanikio hayo yalitangazwa wakati wa hafla ya kufunga maonesho hayo iliyofanyika Viwanja vya Mwahako, Jijini Tanga, leo tarehe 6 Juni 2026, ambapo Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Peter Lyochi alifunga rasmi maonesho hayo yaliyowakutanisha washiriki kutoka sekta mbalimbali za biashara, utalii, elimu na uwekezaji. Kwa siku zote za maonesho hayo yaliyoanza tarehe 28 Mei 2026, banda la Chuo Kikuu Mzumbe limekuwa miongoni mwa maeneo yaliyovutia idadi kubwa ya wageni waliotembelea kupata taarifa kuhusu programu za masomo, kozi fupi, huduma za ushauri wa kitaalamu pamoja na fursa mbalimbali zinazotolewa na Chuo. Moja ya maeneo yaliyopata mwitikio mkubwa kutoka kwa wadau ni taarifa kuhusu Kampasi mpya ya Chuo Kikuu Mzumbe iliyojengwa mkoani Tanga, ambayo inatarajiwa kuanza kutoa huduma za kitaaluma katika siku za usoni. Kupitia maonesho hayo, Chuo kilitumia fursa hiyo kutangaza uwepo wa kampasi hiyo pamoja na fursa za uwekezaji zinazozunguka maendeleo yake, ikiwemo huduma za malazi, biashara, huduma za kijamii na maeneo mengine yatakayochochewa na ongezeko la shughuli za kiuchumi zitakazoambatana na kuanza kwa shughuli za kampasi hiyo. Wakizungumza na wageni waliotembelea banda la Chuo katika nyakati tofauti za maonesho hayo, timu ya Chuo ilieleza kuwa uwekezaji unaozunguka kampasi hiyo mpya unalenga kuifanya Tanga kuwa kitovu muhimu cha elimu ya juu, huku ukifungua fursa mpya za ajira, biashara na maendeleo kwa wananchi wa mkoa huo na maeneo ya jirani. Ushindi wa jumla uliopatikana katika maonesho hayo unaongeza orodha ya mafanikio ya Chuo Kikuu Mzumbe na kuimarisha taswira yake kama taasisi inayoendelea kupanua wigo wa huduma zake za elimu na kuchangia maendeleo ya taifa kupitia miradi ya kimkakati yenye manufaa kwa jamii.