News-Details

News >Details

PROF. HAWA TUNDUI PETRO AWATAKA WANATAALUMA WAPYA MZUMBE KUWA VINARA WA UBORA KATIKA UFUNDISHAJI WA KIDIJITALI

PROF. HAWA TUNDUI PETRO AWATAKA WANATAALUMA WAPYA MZUMBE KUWA VINARA WA UBORA KATIKA UFUNDISHAJI WA KIDIJITALI

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe - Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui Petro amewataka wanataaluma wapya walioajiriwa chuoni hapo kujenga utamaduni wa kujifunza, kutumia teknolojia kwa ufanisi ili kuendelea kuimarisha ubora wa elimu ya juu, wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika leo tarehe, 13 Juni 2026 katika Ukumbi wa Mikutano, Kampasi Kuu ya Chuo hicho, Morogoro. Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Kituo cha Umahiri katika Ufundishaji na Ujifunzaji wa Kibunifu, yamewakutanisha wahadhiri wapya kwa lengo la kuwawezesha kuendana na mabadiliko ya teknolojia, mbinu za kisasa za ufundishaji na mahitaji mapya ya elimu ya juu hususan matumizi ya mfumo wa e-learning. Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Prof. Hawa alieleza kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kujijengea heshima kwa kuzalisha wahitimu wenye ubora, jambo ambalo linapaswa kuendelezwa kupitia ufundishaji unaozingatia matokeo ya ujifunzaji, umahiri wa wanafunzi na matumizi sahihi ya teknolojia. Aidha, Prof. Hawa alisisitiza kuwa jukumu la kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa na ujuzi unaostahili lipo mikononi mwa wahadhiri, huku akiwataka kutumia mafunzo hayo kama fursa ya kuongeza uwezo wao wa kitaaluma na kuendana na mabadiliko yanayoendelea duniani. “Tunataka kuendelea kuzalisha wahitimu wenye ubora ambao watakuwa suluhisho la changamoto za jamii na taifa. Hilo linawezekana pale wahadhiri wanapokuwa tayari kujifunza, kubadilika na kutumia mbinu bunifu katika ufundishaji,” alisema Prof. Hawa. Kwa upande wake, Kaimu Mtiva wa Kitivo cha Sayansi za Jamii, Dkt. Haruni Machumu, alieleza kuwa wahadhiri wa leo wanapaswa kuwa wabunifu, watafiti na wanaojifunza kila wakati ili waweze kuwaongoza wanafunzi katika mazingira yanayobadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya sayansi, teknolojia na uchumi wa maarifa. Naye Mratibu wa Kituo cha Umahiri katika Ufundishaji na Ujifunzaji wa Kibunifu, Dkt. Perpetua Kalimasi, alifafanua kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha washiriki kuelewa na kutumia kwa ufanisi mbinu za kisasa za ufundishaji na tathmini zinazozingatia umahiri wa mwanafunzi. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwasaidia wanataaluma wapya kuimarisha uwezo wao wa kitaaluma, kuongeza ubunifu katika ufundishaji na kuhakikisha Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kuzalisha wahitimu wenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kukabiliana na changamoto za dunia inayobadilika kwa kasi.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None