Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kung’ara katika majukwaa ya kimataifa ya elimu baada ya wanafunzi kutoka Kitivo cha Sheria kushiriki kwa mafanikio katika Mashindano ya Kimataifa ya Midahalo ya Afrika Mashariki Msimu wa Pili, yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Harvard cha Marekani, Shirika la Midahalo na Unenaji wa Ushindani Tanzania (TCRO) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mashindano hayo yaliyofanyika tarehe 12 hadi 14 Juni 2026, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, yaliwakutanisha washiriki kutoka Tanzania, Kenya, Uganda na Marekani katika ushindani wa hoja uliojaa weledi na ubunifu. Katika mashindano hayo, jumla ya timu 24 kutoka vyuo vikuu mbalimbali zilishiriki, zikijadili masuala tofauti ya kijamii, kiuchumi na maendeleo kwa mtazamo wa kina na wa kitaaluma. Timu ya Chuo Kikuu Mzumbe iliyoundwa na Bw. Prince Joseph, Bw. Naseem Maulid, Bi. Gloria Shirima na Bi. Tecla Wegesa ilionesha weledi wa hali ya juu katika mjadala, ikijipambanua kupitia uwezo wa utafiti, uchambuzi wa hoja na uwasilishaji wa kimkakati katika kila hatua ya mashindano. Ushiriki wao uliakisi maandalizi bora ya kitaaluma na uimara wa mafunzo yanayotolewa katika Kitivo cha Sheria. Katika ushindani huo mkali, timu hiyo ilijidhihirisha miongoni mwa vikosi vilivyokuwa na ushawishi mkubwa katika mjadala, ikionesha uwezo wa kushindana kwa ujasiri dhidi ya timu kutoka vyuo vikuu vya ndani na nje ya Tanzania ikiwa ni ishara ya wazi ya kuimarika kwa uwezo wa wanafunzi wa Mzumbe katika majukwaa ya kimataifa ya kitaaluma. Kwa ujumla, ushiriki huo umeendelea kukitangaza vyema Chuo Kikuu Mzumbe kama taasisi inayojenga kizazi cha wataalamu wenye uwezo wa kufikiri kwa kina, kujenga hoja kwa weledi na kushiriki kikamilifu katika mijadala ya kimataifa inayolenga kutafuta suluhisho la changamoto za kijamii na maendeleo endelevu.