News-Details

News >Details

MZUMBE YAPAISHA KISWAHILI KIMATAIFA

MZUMBE YAPAISHA KISWAHILI KIMATAIFA

Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu Mzumbe Bi. Alphonsina Silayo amehitimisha kwa mafanikio programu ya mwezi mmoja ya ufundishaji wa Kiswahili nchini Rwanda, iliyoanza Aprili 24, 2026 hadi Mei 23, 2026, chini ya ufadhili wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki - KAKAMA) ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza na kuimarisha matumizi ya Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki. Katika kipindi cha utekelezaji wa programu hiyo, Bi. Silayo alihudumu katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Rwanda (ICK) ambapo alihusika katika kufundisha Kiswahili kwa wanafunzi na wahadhiri, hatua iliyopokelewa kwa hamasa kubwa na jamii ya kitaaluma kutokana na mchango wake katika kukuza umahiri wa lugha hiyo kama njia ya mawasiliano na elimu. Mbali na jukumu la ufundishaji, Bi. Alphonsina Silayo alikabidhi vitabu 48 vilivyotoka Tanzania ili kusaidia upatikanaji wa rasilimali za kujifunzia Kiswahili. Vilevile, Bi. Silayo alitoa kalamu na skafu zenye utambulisho wa Chuo Kikuu Mzumbe kama ishara ya kuendeleza uhusiano wa kitaaluma na kitamaduni kati ya taasisi hizo mbili. Katika kuendeleza wajibu wa kijamii unaoambatana na taaluma, Bi. Silayo alitembelea Shule ya Sekondari ya St. Joseph na Shule ya Sekondari ya St. Marie Reine nchini Rwanda, ambazo hufundisha Kiswahili kama somo. Akiwa katika shule hizo, Bi. Silayo alitoa mafunzo maalumu kwa wanafunzi na walimu pamoja na kukabidhi vitabu vya kujifunzia Kiswahili, hatua iliyolenga kuhamasisha ujifunzaji wa lugha hiyo na kuimarisha ubora wa ufundishaji wake katika ngazi ya elimu ya sekondari. Kukamilika kwa programu hiyo kunadhihirisha mchango wa Chuo Kikuu Mzumbe katika kuendeleza ajenda ya Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Aidha, kunatoa kielelezo cha namna ushirikiano wa kikanda unavyoweza kuimarisha elimu, kuendeleza utamaduni na kukuza matumizi ya Kiswahili kama lugha inayounganisha jamii za Afrika Mashariki.

None
None
None
None
None
None
None