News-Details

News >Details

KUEHNE FOUNDATION YAWEZESHA ZIARA YA MAFUNZO KIWANDA CHA BAKHRESA

KUEHNE FOUNDATION YAWEZESHA ZIARA YA MAFUNZO KIWANDA CHA BAKHRESA

Katika kuimarisha ujifunzaji unaounganisha nadharia na vitendo, wanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu Mzumbe wanaosoma Shahada ya Kwanza ya Sayansi katika Usimamizi wa Shughuli za Uzalishaji na Uendeshaji (BSc. Production and Operations Management) wametembelea kiwanda cha uzalishaji wa juisi cha Azam kilichopo chini ya Bakhresa Food Products Limited, kwa lengo la kujifunza kwa vitendo mifumo ya kisasa ya uzalishaji na uendeshaji wa viwanda. Ziara hiyo iliyofanyika tarehe 24 Juni 2026, katika mazingira ya kiwanda hicho cha juisi cha Azam jijini Dar es Salaam na kuwezeshwa na Mradi wa Kühne Foundation, iliwapa wanafunzi nafasi ya kuona kwa karibu namna michakato ya uzalishaji inavyopangwa, kusimamiwa na kuendeshwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuongeza ufanisi, ubora na tija katika uzalishaji wa kiwango kikubwa. Katika ziara hiyo, wanafunzi walijifunza kwa vitendo matumizi ya dhana muhimu za usimamizi wa uzalishaji kama vile upangaji wa uzalishaji, matumizi bora ya uwezo wa uzalishaji, mpangilio wa kiwanda, uwiano wa mistari ya uzalishaji na mbinu za uzalishaji makini. Pia, wanafunzi walielezwa kwa kina namna dhana hizo zinavyotumika katika kupanga, kuratibu na kusimamia shughuli za uzalishaji ili kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa ufanisi, upotevu unapunguzwa, tija inaongezeka na mtiririko wa kazi ndani ya kiwanda unakuwa wa kuendelea na wenye ufanisi zaidi. Aidha, wanafunzi hao walielekezwa kuhusu mifumo ya udhibiti wa ubora na usalama wa chakula inayotumika kuhakikisha kuwa bidhaa zote zinazoingia sokoni zinakidhi viwango vinavyotakiwa. Wataalamu wa kiwanda walisisitiza kuwa ubora ni mchakato unaoanzia hatua ya awali ya uzalishaji na kuendelea katika kila hatua hadi bidhaa inapokamilika. Akizungumzia umuhimu wa ziara hiyo, mmoja wa waratibu wa ziara hiyo ya masomo ambaye pia ni Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu Mzumbe Bi. Sophia Mwalongo alisema kuwa mafunzo ya vitendo ni nyenzo muhimu katika kuwaandaa wanafunzi kwa soko la ajira, kwani yanawawezesha kuona kwa macho yao jinsi nadharia zinavyotekelezwa katika mazingira halisi ya kazi. Kwa upande wao, wanafunzi walieleza kuwa ziara hiyo imewasaidia kuelewa kwa undani zaidi taaluma yao na kuwapa mtazamo mpana kuhusu nafasi ya wataalamu wa uzalishaji na uendeshaji katika kuboresha ufanisi wa viwanda na ushindani wa biashara. Waliongeza kuwa uzoefu huo umeongeza hamasa yao ya kujifunza na kujiendeleza kitaaluma. Kwa wanafunzi hao, ziara hiyo haikuwa tu sehemu ya mafunzo ya kitaaluma, bali pia daraja muhimu lililowaunganisha na mazingira halisi ya kazi wanayotarajia kuyaingia baada ya kuhitimu. Uzoefu walioupata unatarajiwa kuwaongezea umahiri wa kitaaluma, kuimarisha uwezo wao wa kutatua changamoto za kiutendaji na kuwajengea msingi imara wa kuwa wataalamu wa uzalishaji na uendeshaji wenye ushindani katika uchumi wa kisasa.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None