Ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utamaduni wa huduma kwa jamii, wanafunzi wa Idara ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa Chuo Kikuu Mzumbe kutoka ngazi zote za masomo yaani Astashahada hadi Shahada ya Umahiri, wamefanya matendo ya huruma kwa Shirika la Childhood Development Organization (CDO), leo tarehe 26 Juni 2026, lilipo Kijiji cha Changarawe, Mzumbe wakitoa msaada wa mahitaji muhimu kwa watoto na wazee wanaohudumiwa na shirika hilo. Katika hafla hiyo, wanafunzi walikabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali muhimu, ikiwemo unga, mchele, sukari, sabuni, mafuta ya kula, mafuta ya kupaka, madaftari, kalamu, penseli, nguo, juisi, biskuti na vifaa vingine vinavyochangia kuboresha ustawi wa watoto na wazee wanaohudumiwa na Shirika la CDO. Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Bw. Fayid Mohamed Yasani, alieleza kuwa tukio hilo limeandaliwa na wanafunzi wa Idara ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa kwa ushirikiano na uongozi wa idara, likiwa na lengo la kuendeleza utamaduni wa kujitolea, kuimarisha mshikamano na jamii, pamoja na kuwajengea wanafunzi uelewa wa kushiriki kikamilifu katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii. Kwa upande wake, Mratibu wa Miradi wa CDO, Bw. Joseph Kazimoto, aliishukuru Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuendelea kushirikiana na shirika hilo kupitia shughuli mbalimbali za kijamii. Bw. Kazimoto alieleza kuwa wanafunzi wa Idara ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa wamekuwa wakitembelea kituo hicho mara kwa mara tangu mwaka 2021, wakitoa misaada na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii. Aidha, Bw. Kazimoto alifafanua kuwa shirika hilo lililoanzishwa mnamo mwaka 1998 lina dhamira ya kuwahudumia watoto wanaotoka katika familia zenye uhitaji kwa kuwapatia elimu, mahitaji muhimu ya kujifunzia na kuwawezesha kutimiza ndoto zao za maisha. Aliongezea kuwa shirika hilo limeendelea kutoa mafunzo ya stadi za maisha, kupokea wanafunzi wa mafunzo kwa vitendo kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya juu, kushirikiana na wadau wa maendeleo na kutekeleza miradi inayolenga kuboresha ustawi wa jamii. Naye Mkuu wa Idara ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Denis Kamugisha, aliwapongeza wanafunzi kwa moyo wa kujitolea waliouonesha katika kuandaa hafla hiyo, akisisitiza kuwa elimu inayotolewa chuoni inapaswa kuonekana kupitia vitendo vinavyoleta manufaa kwa jamii. "Elimu tunayotoa hapa Chuo Kikuu Mzumbe inapaswa kuwajenga wanafunzi kuwa wataalamu wenye uwezo wa kutumia maarifa yao kutatua changamoto za jamii. Matendo kama haya ndiyo yanayoonesha thamani halisi ya elimu na mchango wa chuo katika maendeleo ya taifa," alisema Prof. Kamugisha. Kwa kuendelea kushiriki katika shughuli za aina hii, Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kujenga kizazi cha wataalamu wanaotambua wajibu wao kwa jamii na wanaoweza kutumia taaluma zao kuleta suluhisho kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.