News-Details

News >Details

WANAFUNZI MZUMBE WAPATIWA MAARIFA YA VITENDO KUHUSU UTAWALA WA SERIKALI ZA MITAA

WANAFUNZI MZUMBE WAPATIWA MAARIFA YA VITENDO KUHUSU UTAWALA WA SERIKALI ZA MITAA

Chuo Kikuu Mzumbe kimeendesha Mhadhara wa Umma ulioandaliwa na Idara ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa, uliowakutanisha wanataaluma, wanafunzi na wadau mbalimbali katika Kampasi Kuu ya Morogoro tarehe 26 Juni 2026. Mhadhara huo uliwasilishwa na mtaalamu wa utawala wa umma na mhitimu wa chuo hicho, Bw. Rashid Mfaume Taka, akijikita katika uchambuzi wa utendaji wa serikali za mitaa, mwelekeo wake, changamoto na fursa katika muktadha wa mageuzi ya utawala wa umma nchini Tanzania. Akiwasilisha mada yake, Bw. Rashid Mfaume Taka aliwahimiza wanafunzi kutazama kwa mapana dhana ya utendaji wa serikali za mitaa, akieleza kuwa mafanikio hayawezi kupimwa kwa miundombinu pekee kama ujenzi wa madarasa au hospitali, bali yanapaswa kuzingatia malengo ya msingi ya mfumo huo ikiwemo ushirikishwaji wa wananchi, uboreshaji wa huduma, demokrasia na utawala bora. Bw. Taka alisisitiza pia umuhimu wa uchambuzi wa kina unaounganisha sera, historia na uhalisia wa utekelezaji ili kupata taswira sahihi ya maendeleo. Aidha, Bw. Taka aliwahimiza wanafunzi kujijengea umahiri wa kitaaluma na kiutendaji, akisisitiza kuwa ushindani katika soko la ajira unahitaji zaidi ya maarifa ya darasani pekee, bali pia ubunifu, uwezo wa kuchanganua masuala na kujifunza kwa kujiongeza ili kuendana na mabadiliko ya sekta ya utawala wa umma. Awali, Mkuu wa Idara ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa, Prof. Denis Kamugisha, alimtambulisha Bw. Taka kama mhitimu mwenye historia pana ya kitaaluma na kiutendaji, aliyewahi kuhudumu kama mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe, kiongozi wa idara, mratibu wa programu za kimataifa, na baadaye Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro. Prof. Kamugisha alibainisha kuwa uzoefu huo unampa uwezo wa kipekee wa kuchambua masuala ya utawala wa umma kwa mtazamo wa kitaaluma na kiutendaji. Mhadhara huo ulihitimishwa kwa msisitizo wa kuendeleza mijadala ya kitaaluma ndani na nje ya darasa, huku wanafunzi wakihimizwa kutumia maarifa waliyojifunza kuchambua kwa kina mifumo ya utawala wa umma na utendaji wa serikali za mitaa kwa mtazamo wa kitaaluma na kiutendaji.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None