News-Details

News >Details

MZUMBE YASHIRIKI MAONESHO YA 13 YA BIASHARA NA UTALII YA TANGA

MZUMBE YASHIRIKI MAONESHO YA 13 YA BIASHARA NA UTALII YA TANGA

Chuo Kikuu Mzumbe ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki Maonesho ya 13 ya Biashara na Utalii ya Tanga yanayofanyika Jijini Tanga kuanzia tarehe 28 Mei hadi 6 Juni 2026. Maonesho hayo yamewakutanisha taasisi mbalimbali za umma na binafsi kwa lengo la kuonesha huduma, bidhaa na fursa za uwekezaji zinazochangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii, yakiwa na kaulimbiu isemayo; “Kuonesha Sekta ya Kimkakati ya Mabadiliko ya Kiuchumi Kuunga Mkono Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.” Akifungua rasmi maonesho hayo, Mgeni rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhe. Ayubu Sebabili, amesema maonesho hayo ni jukwaa muhimu la kutangaza fursa zilizopo katika Mkoa wa Tanga na kuvutia wawekezaji pamoja na wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi. Mhe. Sebabili amekipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushiriki maonesho hayo na kutumia jukwaa hilo kutangaza fursa mbalimbali zinazopatikana chuoni pamoja na Kampasi ya Tanga iliyopo wilayani Mkinga. Aidha aliongeza kuwa ushiriki wa chuo katika maonesho hayo unaunga mkono juhudi za Mkoa wa Tanga za kutangaza fursa za maendeleo, huku ukichangia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma za elimu, utafiti na fursa za uwekezaji zinazopatikana katika chuo hicho. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) Mkoa wa Tanga, Bw. Rashid Mwanyoka, amesema maonesho hayo ni sehemu ya mikakati ya kukuza biashara, utalii na uwekezaji katika Mkoa wa Tanga. Ameeleza kuwa mkoa huo una fursa nyingi za kiuchumi zinazotokana na uwepo wa bandari, miradi mikubwa ya kimkakati pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji yanayoendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Ushiriki wa Chuo Kikuu Mzumbe katika maonesho haya, umeongeza fursa ya elimu kwa wananchi kuhusu programu mbalimbali za masomo, shughuli za utafiti, huduma za ushauri na fursa zinazopatikana Chuoni hapo. Aidha kwa upekee Chuo kinatumia maonesho hayo kuzinadi fursa za kiuwekezaji zinazopatikana katika Kampasi ya Tanga iliyopo wilayani Mkinga, Kijiji cha Gombero, kwa lengo la kuvutia wadau mbalimbali kushiriki katika maendeleo yake.

None
None
None
None
None
None
None