News-Details

News >Details

TAASISI YA UONGOZI YAWAKUTANISHA VIJANA KATIKA KONGAMANO KUBWA

TAASISI YA UONGOZI YAWAKUTANISHA VIJANA KATIKA KONGAMANO KUBWA

Taasisi ya Uongozi Tanzania (Tanzania Leadership Foundation - TLF) imeandaa Kongamano la Vijana la Uongozi lililofanyika leo tarehe 20 Juni 2026 katika Ukumbi wa Samora, Kampasi Kuu Morogoro, likiwakutanisha mamia ya vijana kutoka sehemu mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uwezo wa uongozi, uzalendo, ubunifu na ushiriki katika maendeleo ya Taifa. Akifungua kongamano hilo, Mgeni Rasmi ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, aliwahimiza vijana kutokata tamaa katika safari ya maisha na maendeleo. Aliwataka kuwa wabunifu, wachapakazi, wanyenyekevu na wazalendo, huku akisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua na kutumia fursa zilizopo ili kufikia malengo yao na kuchangia maendeleo ya nchi. Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, alisema kongamano hilo limekuja wakati muafaka wa kuwaandaa vijana kwa dunia inayobadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia na akili mnemba (AI). Aliwahimiza vijana kutumia fursa ya kujifunza kutoka kwa viongozi na wataalamu mbalimbali waliokuwepo katika kongamano hilo ili kujenga maono yatakayowawezesha kuiongoza Tanzania katika miaka ijayo. Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Uongozi Tanzania (TLF) ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Jabiri Makame, alisema lengo kuu la taasisi hiyo ni kuandaa kizazi cha viongozi wenye maadili, uzalendo na uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika sekta za umma na binafsi. Alibainisha kuwa kongamano hilo ni sehemu ya juhudi za kuwaandaa vijana kwa nafasi za uongozi na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa. Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Prof. Hawa Petro Tundui, akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo, alisema kongamano hilo linaendana na kaulimbiu ya Chuo ya “Kujifunza kwa Maendeleo ya Watu” kwa kuwawezesha vijana kupata maarifa, stadi na maadili yatakayowasaidia kuwa viongozi wenye mchango chanya katika jamii na Taifa kwa ujumla. Katika kongamano hilo, washiriki walipata fursa ya kusikiliza mada mbalimbali zilizowasilishwa na viongozi wa Serikali, wataalamu, wakufunzi na wanajasiriamali kuhusu uongozi, maendeleo ya vijana, ujasiriamali, matumizi ya teknolojia na maadili. Washiriki walihimizwa kutumia maarifa waliyojifunza kujenga uwezo wao wa uongozi, ubunifu na uzalendo ili kuwa sehemu ya maendeleo endelevu ya Taifa.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None