News-Details

News >Details

MZUMBE YAZUNGUMZIA NAFASI YA PPP KATIKA KUCHOCHEA UWEKEZAJI NA MAENDELEO YA TAIFA

MZUMBE YAZUNGUMZIA NAFASI YA PPP KATIKA KUCHOCHEA UWEKEZAJI NA MAENDELEO YA TAIFA

Kwa kuzingatia umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi katika kukuza uchumi na kuongeza uwekezaji, Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Skuli ya Biashara kimeandaa Mhadhara wa Umma uliolenga kujadili nafasi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership - PPP) katika kufanikisha ajenda za maendeleo ya Taifa. Mhadhara huo wenye mada isemayo “Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP): Nguzo ya Kimkakati katika Kugharamia Mpango wa Nne wa Maendeleo na Dira ya 2050” umefanyika leo tarehe 26 Juni 2026 katika Ukumbi wa Samora, Kampasi Kuu Morogoro, ukiwakutanisha viongozi, wanataaluma, wanafunzi na wadau mbalimbali wa maendeleo. Akiwasilisha mada yake, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), Bw. David Kafulila, alisema mfumo wa PPP ni nyenzo muhimu inayowezesha Serikali na sekta binafsi kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuongeza mitaji, ubunifu na ufanisi wa utoaji wa huduma kwa jamii. Bw. Kafulila alieleza kuwa ushirikiano huo una nafasi kubwa katika kujenga uchumi unaozalisha ajira na kuongeza tija kwa Taifa. Aidha, alisisitiza umuhimu wa taasisi za elimu ya juu kufanya tafiti, kutoa maarifa na kuwaandaa vijana kuelewa fursa zinazotokana na PPP. Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, alisema PPP ni jukwaa muhimu la kuunganisha nguvu za Serikali na sekta binafsi katika kuongeza uwekezaji, ubunifu na fursa za ajira nchini. Prof. Mwegoha alibainisha kuwa taasisi za elimu ya juu zina nafasi ya kipekee katika kujenga uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa ubia huo kupitia ufundishaji, tafiti na ubunifu wa kutafuta suluhisho kwa changamoto za maendeleo. Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui Petro, alisema mhadhara huo umeongeza fursa kwa wanataaluma na wanafunzi kupata maarifa kuhusu mchango wa PPP katika maendeleo ya Taifa. Alieleza kuwa eneo hilo lina umuhimu katika kuimarisha ufundishaji, utafiti na kujenga uwezo wa wataalamu watakaoshiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Akizungumza katika mhadhara huo, Amidi wa Skuli ya Biashara ya Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Gabriel Vitus Komba, alisema majukwaa ya kitaaluma ni muhimu katika kuunganisha maarifa ya darasani na utekelezaji wa miradi halisi ya maendeleo. Aliongeza kuwa mijadala hiyo huwasaidia wanafunzi na wanataaluma kuelewa fursa, changamoto na mikakati ya kutumia PPP kama chombo cha kuongeza uwekezaji na kuimarisha uchumi wa Taifa. Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha uzalishaji wa maarifa, tafiti na mafunzo yenye mchango katika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi, sambamba na kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kuchochea maendeleo kupitia ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za elimu ya juu.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None