News-Details

News >Details

WAJUMBE WA BARAZA LA CHUO KIKUU MZUMBE WAJENGEWA UWEZO KATIKA UONGOZI NA UTAWALA BORA

WAJUMBE WA BARAZA LA CHUO KIKUU MZUMBE WAJENGEWA UWEZO KATIKA UONGOZI NA UTAWALA BORA

Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kuwekeza katika kuimarisha mifumo ya utawala wa taasisi kwa kuwajengea uwezo wajumbe wa Baraza lake la 10 kupitia mafunzo ya siku mbili kuhusu uongozi wa bodi, utawala bora na usimamizi wa kimkakati. Mafunzo hayo yameanza leo tarehe 01 Julai 2026 katika Hoteli ya Tanga Beach Resort, mkoani Tanga, yakileta pamoja wajumbe na sekretarieti ya Baraza la Chuo na wataalamu mbalimbali wa masuala ya utawala wa taasisi. Akifungua mafunzo hayo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha alieleza kuwa Baraza la Chuo lina nafasi ya msingi katika kusimamia maendeleo ya taasisi, hivyo ni muhimu kwa wajumbe wake kuendelea kuimarisha uelewa kuhusu masuala ya utawala bora, mifumo ya usimamizi na majukumu yao ya kisheria ili kufanya maamuzi yenye tija yanayochochea maendeleo endelevu ya Chuo. Alieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya dhamira ya Chuo ya kuhakikisha Baraza linaendelea kuwa na uwezo wa kusimamia utekelezaji wa mipango ya kimkakati kwa kuzingatia misingi ya uwazi, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali. Mwezeshaji kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Hussein Ally Kakurwa, aliwasilisha mada kuhusu majukumu ya Bodi za Wakurugenzi na mgawanyo wa majukumu kati ya Bodi na Mamlaka nyingine katika Usimamizi wa Taasisi na Mashirika ya Umma. Katika wasilisho lake, alifafanua nafasi na wajibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina katika usimamizi wa taasisi za umma, majukumu ya bodi za wakurugenzi na mabaraza, wajibu wa kila mjumbe wa bodi pamoja na mgawanyo wa majukumu kati ya bodi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wizara mama na mamlaka nyingine za usimamizi. Aidha, Bw. Kakurwa alieleza changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri utendaji wa bodi, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uongozi na ushirikiano katika kufanya maamuzi yanayolenga kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa taasisi za umma. Kwa upande wake, Mwezeshaji ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Bandari, Dkt. Lufunyo S. Hussein, aliwasilisha mada kuhusu Utawala Bora, Uongozi na Usimamizi wa kimkakati kwa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe, akijikita katika umuhimu wa uongozi wenye maono, usimamizi wa kimkakati, uwajibikaji na ufuatiliaji wa utekelezaji wa malengo ya taasisi. Alisisitiza kuwa wajumbe wa baraza wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, kufanya maamuzi yanayolinda maslahi ya taasisi na kuhakikisha mipango ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi. Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Chuo Kikuu Mzumbe za kuhakikisha vyombo vyake vya maamuzi vinaendelea kuwa na uwezo wa kusimamia taasisi kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, uwazi, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali kwa manufaa ya Chuo na wadau wake.

None
None
None
None
None
None