Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kuimarisha uwezo wa chombo chake kikuu cha maamuzi kwa kuwajengea uwezo wajumbe wa Baraza na Sekretarieti ya Baraza katika maeneo ya uongozi wa kimkakati, utawala bora na usimamizi wa rasilimali za umma. Mafunzo hayo ya siku mbili yamehitimishwa leo, tarehe 02 Julai 2026, katika Hoteli ya Tanga Beach Resort, mkoani Tanga, ni sehemu ya mkakati wa Chuo wa kuendelea kujenga uongozi wenye maono na uwajibikaji unaosimamia maendeleo ya taasisi kwa ufanisi. Akifunga mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe, Balozi Modest Jonathan Mero, amewataka wajumbe wa Baraza kuyatumia maarifa na uzoefu walioupata kama nyenzo ya kuimarisha utendaji wa Baraza na kufanya maamuzi yenye tija kwa maendeleo ya Chuo. Alieleza kuwa mafunzo hayo yameimarisha msingi wa Baraza katika kutekeleza majukumu yake kwa weledi, kufanya maamuzi yanayozingatia maslahi mapana ya taasisi na kuendeleza utamaduni wa kujifunza unaochochea ubunifu, uwajibikaji na maendeleo endelevu. Aidha, Balozi Mero aliwashukuru wawezeshaji kwa maarifa waliyoyawasilisha pamoja na wajumbe wa Baraza na Sekretarieti kwa ushiriki wao na kujitolea katika kipindi chote cha mafunzo. Miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mafunzo hayo ni uongozi unaozingatia akili hisia, ambapo wajumbe wa Baraza walijengewa uwezo kuhusu nafasi ya akili hisia katika kuimarisha ufanisi wa vyombo vya maamuzi na usimamizi wa taasisi mada iliyowasilishwa na mtaalamu wa uongozi, utawala bora na ujifunzaji kwa njia ya kielektroniki (e-Learning), Bw. Charles Senkondo. Kwa upande wake, Kaimu Msajili Idara ya Fedha na Utawala - Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), CPA Paul Bilabaye aliwasilisha mada kuhusu uongozi katika usimamizi wa rasilimali za umma, akisisitiza kuwa uwajibikaji, uadilifu, uzingatiaji wa sheria na matumizi bora ya rasilimali ni msingi wa taasisi imara na zinazotekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Alibainisha kuwa viongozi wanapaswa kusimamia rasilimali kwa mtazamo wa kuongeza thamani na kuhakikisha kila uamuzi unaunga mkono malengo ya kimkakati ya taasisi. Kupitia uwekezaji huo katika maendeleo ya uwezo wa viongozi wake, Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kuimarisha mifumo ya uongozi na utawala inayowezesha utekelezaji madhubuti wa mipango yake ya kimkakati, huku kikihakikisha Baraza linaendelea kuwa nguzo muhimu katika kusukuma mbele dira na malengo ya Chuo.