Chuo Kikuu Mzumbe kimeshiriki katika uandaaji wa Semina ya Kuendeleza Uwezo wa Tathmini Tanzania 2025: Mustakabali wa Tathmini, semina hii imefanyika katika Chuo Kikuu cha Ardhi Dar es Salaam, Tanzania kuanzia tarehe 25 hadi 27 Februari 2025. Tukio muhimu limewaleta pamoja watunga sera, watafiti, wasomi na wataalamu wa maendeleo kujadili mustakabali wa tathmini. Semina hii imeandaliwa na Ofisi Maalum ya Tathmini - Ubelgiji, IOB (Chuo Kikuu cha Antwerp) na Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Mradi wa MU-IOB ICP Connect, semina hii inatoa jukwaa la kushiriki maarifa, kujenga uwezo, na kushirikiana kati ya wataalamu wa ndani na wa kimataifa. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina hiyo, Mwenyekiti wa IOB, Prof. Nathalie Holvet amesema kuwa semina hii yenye kaulimbiu “Mustakabali wa Tathmini”, inalenga kuimarisha uwezo wa kitaifa katika ufuatiliaji na tathmini (M&E) na kuendeleza maamuzi yanayozingatia ushahidi katika sekta mbalimbali. Semina iliendelea kwa majadiliano yaliyohusisha mada muhimu za tathmini, zikiwemo Kuasilisha Tathmini kwa Muktadha wa Kiasili, Tathmini Inayozingatia Usawa, Tathmini ya Mifumo Changamano, Ramani Shirikishi za Mifumo, na Ushirikiano wa Teknolojia ya Zamani na Mpya katika Tathmini. Kwa kuzingatia changamoto za kimataifa za mabadiliko ya tabianchi, semina pia imechunguza Tathmini na Mabadiliko ya Tabianchi, ikihusisha mchango wa M&E katika kushughulikia changamoto za mazingira. Vilevile, msisitizo umewekwa katika Kuhusisha Tathmini katika Mfumo wa Serikali, kuhakikisha kwamba M&E inakuwa sehemu muhimu ya uundaji na utekelezaji wa sera. Akizungumza kabla ya tukio hilo, mwakilishi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Christina Shitima alisisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa tathmini nchini Tanzania. “Semina hii ni fursa adhimu ya kuendeleza mifumo yetu ya kitaifa ya ufuatiliaji na tathmini. Kwa kutumia mbinu za tathmini za jadi na za kisasa, tunaweza kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inapimwa kwa ufanisi na inaboreshwa mara kwa mara,” alisema Dkt. Shitima. Semina ya Kuendeleza Uwezo wa Tathmini 2025 imehushisha washiriki kutoka taasisi za serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyuo vikuu, na mashirika ya maendeleo ya kimataifa ikiwemo nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burkina Faso, Comoro, Morocco, Nicaragua, Benin, Mali, Cameroon, Moldova, Msumbiji, Palestina na Ubelgiji. Matokeo ya semina hii yanatarajiwa kuchangia pakubwa katika kuboresha mbinu za tathmini nchini Tanzania na kwingineko.