Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe, Balozi Modest Jonathan Mero, amesisitiza umuhimu wa kukamilishwa kwa wakati kwa ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu Mzumbe mkoani Tanga, akieleza kuwa mradi huo ni uwekezaji wa kimkakati utakaopanua fursa za elimu ya juu, kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga na maeneo ya jirani. Hayo ameyasema leo, Julai 04, 2026, katika Kata ya Gombero, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, alipowaongoza wajumbe wa Baraza la Chuo na Sekretarieti ya Baraza kukagua maendeleo ya ujenzi wa kampasi hiyo. Katika ziara hiyo, Balozi Mero aliambatana na wajumbe na Sektretarieti ya Baraza la Chuo akiwemo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, Manaibu Makamu Mkuu wa Chuo, pamoja na baadhi ya waratibu wa Mradi wa HEET, ambapo walitembelea na kukagua majengo mbalimbali yanayojengwa pamoja na miundombinu inayounda kampasi hiyo mpya. Baada ya kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi, Balozi Mero aliipongeza Menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe na Timu ya Mradi wa HEET kwa usimamizi makini uliochangia kufikiwa kwa hatua kubwa ya utekelezaji wa ujenzi huo. Alisema mafanikio hayo yanaakisi dhamira ya Chuo ya kuhakikisha miradi ya maendeleo inasimamiwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa Aidha, alimpongeza mkandarasi kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika na kwa kuzingatia ubora wa ujenzi, huku akimtaka kuongeza nguvu katika kazi zilizobaki ili kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda wa nyongeza uliotolewa, ambao unatarajiwa kumalizika Julai 30, 2026. Kadhalika, aliagiza kuharakishwa kwa taratibu za uwekezaji katika maeneo yanayozunguka kampasi ili kuandaa mazingira rafiki kwa wawekezaji. Alisema uwekezaji katika nyumba za wageni, benki, migahawa, maduka na huduma nyingine utasaidia kukidhi mahitaji yatakayotokana na kuanza kwa shughuli za kampasi na wakati huo huo kuchochea uchumi wa eneo hilo. Kwa mujibu wa taarifa ya maendeleo ya mradi iliyowasilishwa na Mratibu wa Mradi wa HEET anayesimamia Mradi wa Ujenzi wa Kampasi ya Tanga Qs. Prosper Leonard, ujenzi umefikia wastani wa asilimia 91 kwa Lot 1 na asilimia 90 kwa Lot 2. Mradi huo unajumuisha ujenzi wa jengo la utawala na taaluma, ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa watu 300, maabara, madarasa, kituo cha afya, bwalo la chakula lenye uwezo wa kuhudumia watu 450 kwa wakati mmoja, mabweni mawili ya wanafunzi, nyumba za watumishi pamoja na miundombinu ya maji safi, maji taka na usimamizi wa taka ngumu. Kwa kukamilika kwa mradi huu, Chuo Kikuu Mzumbe kitaongeza uwezo wake wa kuhudumia wanafunzi wengi zaidi, kutoa mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, pamoja na kuendelea kuwa mshirika muhimu wa Serikali katika kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi na ushindani.