News-Details

News >Details

KAMATI YA MAPOKEZI YA WANAFUNZI MZUMBE YAACHA ALAMA KWA KUCHANGIA DAMU KUOKOA MAISHA

KAMATI YA MAPOKEZI YA WANAFUNZI MZUMBE YAACHA ALAMA KWA KUCHANGIA DAMU KUOKOA MAISHA

Jumla ya chupa 23 za damu zimekusanywa kufuatia zoezi la hiari la uchangiaji damu lililofanywa na wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe kama sehemu ya kuhitimisha shughuli za Kamati ya Mapokezi ya Wanafunzi wa Mwaka wa Kwanza (Ask Me 2025/2026), hatua inayodhihirisha dhamira ya wanafunzi hao ya kutumia elimu yao kuleta mchango chanya kwa jamii. Zoezi hilo limefanyika Kata ya Mlali wilayani Mvomero, tarehe 4 Julai 2026, katika Kituo cha Afya Mlali. Katika zoezi hilo, wanafunzi 32 walijitokeza kwa hiari kuchangia damu, ambapo chupa 23 zilikusanywa na kukabidhiwa kwa wataalamu wa afya kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo. Damu hiyo inatarajiwa kusaidia kuokoa maisha ya waathirika wa ajali, akina mama wanaopoteza damu wakati wa kujifungua pamoja na watoto wenye upungufu mkubwa wa damu. Uongozi wa Kamati ya Ask Me 2025/2026 ulieleza kuwa lengo lilikuwa kuhitimisha programu ya mapokezi ya wanafunzi kwa kuacha alama yenye manufaa kwa jamii, badala ya kuishia katika shughuli za kawaida za chuoni. Uongozi huo ulisisitiza kuwa uchangiaji damu ni sehemu ya kuwajenga wanafunzi kuwa viongozi wanaotambua wajibu wao kwa jamii na kuthamini uhai wa wengine. Mbali na uchangiaji damu, wadau wa maendeleo kutoka Pathfinder International walitoa elimu kwa wanafunzi kuhusu afya ya uzazi, afya ya vijana na umuhimu wa kufanya maamuzi sahihi yanayochangia ustawi wa maisha yao. Wawakilishi wa taasisi hiyo waliwapongeza wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa moyo wao wa kujitolea, wakieleza kuwa kitendo hicho kinaakisi uwajibikaji wa kijamii na uzalendo unaopaswa kuwa sehemu ya maadili ya wahitimu wa elimu ya juu. Kupitia moyo huo wa kujitolea, wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe wametoa ujumbe kwamba mchango mkubwa zaidi wa msomi haupimwi kwa cheti pekee bali kwa uwezo wake wa kugusa na kuboresha maisha ya wengine.

None
None
None
None