Tafiti na mchango wa Chuo Kikuu Mzumbe katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili vimeendelea kupata utambuzi katika ngazi ya kimataifa baada ya wanataaluma wake kushiriki na kuwasilisha kazi za kitaaluma katika Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili, lililowakutanisha wataalamu, watunga sera na wadau wa Kiswahili kutoka mataifa mbalimbali duniani. Kongamano hilo, lililofanyika kuanzia Julai 4 hadi 7, 2026, jijini Paris lilikuwa sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani (MASIKIDU), yanayoadhimishwa kila mwaka Julai 7 chini ya uratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). Maadhimisho ya mwaka huu yaliongozwa na kaulimbiu isemayo "Kiswahili ni Tunu kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Uchumi Duniani," ikisisitiza nafasi ya lugha hiyo kama nyenzo ya kuunganisha jamii, kukuza utamaduni na kuimarisha mahusiano ya kimataifa. Chuo Kikuu Mzumbe kiliwakilishwa na Mhadhiri Mwandamizi Dkt. Adria Fuluge pamoja na Mhadhiri Msaidizi Bi. Alpha Kavishe kutoka Idara ya Lugha na Stadi za Mawasiliano, Kitivo cha Sayansi za Jamii (FSS). Wataaluma hao walikuwa miongoni mwa washiriki waliochaguliwa kuwasilisha tafiti zao katika kongamano hilo, wakitoa mchango unaoakisi ubora wa tafiti zinazofanywa na Chuo katika taaluma ya Kiswahili. Dkt. Fuluge aliwasilisha utafiti uliobainisha namna muziki wa Kiswahili unavyokuwa daraja la kuunganisha tamaduni na kueneza utambulisho wa Afrika katika jukwaa la dunia. Kwa upande wake, Bi. Alpha aliwasilisha makala iliyochambua mchango wa lugha katika kujenga utamaduni wa amani, mshikamano wa kitaifa na mawasiliano yenye tija. Katika mwendelezo wa ushiriki wake, Dkt. Fuluge pia alikiwakilisha Chuo katika kipindi maalumu cha majadiliano kilichorekodiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Radio Deutsche Welle (DW) ya Ujerumani. Majadiliano hayo yalijadili mada ya "Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani na Mustakabali wa Lugha ya Kiswahili Kimataifa," ambapo washiriki walisisitiza umuhimu wa kuendeleza tafiti, matumizi na ufundishaji wa Kiswahili ili kiendelee kuwa lugha yenye ushawishi katika elimu, diplomasia, biashara na maendeleo ya kijamii duniani. Sambamba na shughuli za kongamano, ujumbe wa Chuo Kikuu Mzumbe ulifanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika UNESCO, Mhe. Dkt. Saidi Othmani Yakubu, kuhusu fursa za ushirikiano katika kufundisha Kiswahili kwa wageni nchini Ufaransa na katika nchi nyingine anazowakilisha. Mazungumzo hayo yanatarajiwa kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kitaaluma na kuendelea kuitangaza Mzumbe kama moja ya taasisi zinazotoa elimu ya Kiswahili kwa viwango vya kimataifa. Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ngazi za juu nchini na jumuiya ya kimataifa, akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pia walihudhuria viongozi wa UNESCO, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu pamoja na Wawakilishi wa taasisi na mashirika mbalimbali yaliyoshiriki kujadili nafasi ya Kiswahili katika dunia ya sasa. Ushiriki wa Chuo Kikuu Mzumbe katika kongamano hilo ni kielelezo cha kukua kwa hadhi ya Chuo katika nyanja za lugha na mawasiliano, huku ukiimarisha taswira yake kama taasisi inayoshiriki kikamilifu katika mijadala ya kimataifa kuhusu maendeleo ya Kiswahili.