News-Details

News >Details

MZUMBE YAWAFIKIA MAELFU YA WADAU SABASABA 2026

MZUMBE YAWAFIKIA MAELFU YA WADAU SABASABA 2026

Chuo Kikuu Mzumbe kimehitimisha kwa mafanikio ushiriki wake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba 2026), baada ya kuwafikia maelfu ya wadau kupitia utoaji wa huduma za udahili, ushauri wa kitaaluma, utafiti, ubunifu na huduma nyingine zinazolenga kuchochea maendeleo ya elimu ya juu na jamii kwa ujumla. Katika kipindi chote cha maonesho yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai, Chuo kilitoa huduma za ushauri kuhusu programu za Astashahada, Stashahada, Shahada na Shahada za Uzamili, huku wataalamu wake wakitoa mwongozo wa udahili kwa wanafunzi watarajiwa na kuwasaidia kukamilisha maombi yao. Wageni waliotembelea banda la Chuo pia walipata fursa ya kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na Mzumbe katika nyanja za utafiti, ubunifu, ushauri wa kitaalamu, huduma za msaada wa kisheria, umataifishaji na shughuli za Baraza la Wahitimu. Mbali na kutoa huduma kwa wananchi, banda la Chuo lilitembelewa na viongozi mbalimbali wa Serikali, taasisi za umma na binafsi, washirika wa maendeleo, wahitimu wa Chuo na wadau kutoka sekta tofauti, waliopata fursa ya kujionea mafanikio ya Chuo na kubadilishana mawazo kuhusu fursa za ushirikiano katika maeneo ya elimu, utafiti, ubunifu na maendeleo ya rasilimali watu. Aidha, ushiriki wa Chuo katika maonesho hayo uliendelea kuimarisha uhusiano na wahitimu wake kupitia kampeni ya usajili wa Baraza la Wahitimu pamoja na utoaji wa elimu kuhusu Mfuko wa Ufadhili wa Masomo wa Jumuiya ya Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe. Wahitimu wengi waliotembelea banda hilo walijisajili na kuonesha utayari wao wa kuendelea kushiriki katika maendeleo ya Chuo. Chuo Kikuu Mzumbe kinawashukuru wanafunzi watarajiwa, wazazi, walezi, wahitimu, washirika wa maendeleo, taasisi mbalimbali na wananchi wote waliotembelea banda lake katika Maonesho ya 50 ya Sabasaba mwaka huu, 2026. Mwitikio huo umeendelea kuimarisha azma ya Chuo ya kuwa taasisi inayoongoza katika kuzalisha maarifa, kuandaa wataalamu mahiri na kutoa mchango endelevu katika maendeleo ya Taifa.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None