News-Details

News >Details

MZUMBE YAWAWEZESHA WATAALAMU MBINU ZA KISASA ZA MAWASILIANO YA TAASISI

MZUMBE YAWAWEZESHA WATAALAMU MBINU ZA KISASA ZA MAWASILIANO YA TAASISI

Katika kuendelea kujibu mahitaji ya maendeleo ya taaluma na mazingira ya kisasa ya kazi, Chuo Kikuu Mzumbe kimeendesha mafunzo ya muda mfupi kuhusu mawasiliano ya taasisi, ushirikishwaji wa wateja na kuongeza tija mahali pa kazi. Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoanza leo tarehe 15 Julai 2026, katika Hoteli ya Morena, yanawaleta pamoja washiriki kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi. Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mwezeshaji ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Stephen Nalaila aliwasilisha mada zilizojikita katika mawasiliano ya kimkakati, maadili ya mawasiliano mahali pa kazi, mbinu za kuboresha mahusiano na wateja, pamoja na matumizi ya mawasiliano kama nyenzo ya kuongeza tija na ufanisi wa taasisi. Aidha, Dkt. Nalaila alieleza kuwa katika mazingira ya sasa ya kazi, mawasiliano si njia ya kubadilishana taarifa pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kuimarisha uongozi, kuongeza uwajibikaji na kujenga taswira chanya ya taasisi. Mafunzo hayo pia yaliwapatia washiriki uelewa kuhusu maadili ya mawasiliano mahali pa kazi, matumizi ya teknolojia katika mawasiliano ya kisasa, mbinu za kushughulikia migogoro ya mawasiliano, uandishi wa nyaraka za kitaalamu pamoja na mbinu za kuwasilisha taarifa kwa ufanisi katika mazingira ya kikazi. Aidha, washiriki walikumbushwa umuhimu wa kuzingatia kanuni na taratibu za mawasiliano katika utumishi wa umma ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kuimarisha ushirikiano ndani ya taasisi. Katika kipindi ambacho taasisi nyingi zinakabiliwa na mabadiliko ya teknolojia, matarajio makubwa ya wadau na ushindani wa utoaji wa huduma, mafunzo hayo yanakuja kama jukwaa muhimu la kuwajengea washiriki uwezo wa kuwasiliana kwa ufanisi, kuongoza mabadiliko na kujenga taasisi zenye uwajibikaji, ubunifu na tija. Chuo Kikuu Mzumbe kitaendelea kubuni na kutoa mafunzo yanayolenga kuendeleza taaluma na kuchangia maendeleo endelevu ya sekta mbalimbali nchini.

None
None
None
None
None
None